December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

zena chitwanga

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma. MAMLAKA ya Serikali Mtandao(e-GA)imesema katika kuhakikisha wanaijenga Serikali ya Kidijiti, Katika kipindi cha miaka 10 ijayo,itaandaa na kutekeleza mikakati madhubuti ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 23,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo.Mha.Ndomba ameeleza kuwa mikakati hiyo ni pamoja na kuwa Sehemu moja ambayo huduma mtandao zote zitakuwa zinapatikana,Uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka, hasa zile za akili bandia, sarafu za kidijiti na teknolojia za kifedha, ili kuwezesha maboresho ya kiutendaji katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa Umma.”Pia Uzalishaji wa vifaa na miundombinu ya TEHAMA (Hardware) ndani ya Tanzania pamoja na Mifumo na miundombinu ya Serikali mtandao iliyobora na imara zaidi,”amesema.Mha.Ndomba amefafanua kuwa ili kufikia yote hayo katika kipindi kijacho, Mamlaka imepanga kushughulikia maeneo ya kipaumbele kama kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi zote za umma, ikiwa ni pamoja na kupitia na kukagua miradi na Mifumo ya TEHAMA ya kimkakati, kisekta na kitaasisi ili kuhakikisha kuwa imetengenezwa na inatumika kwa kufuata Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo iliyopo na kushauri maeneo ya kuboresha na kufuatilia utekelezaji wake.Pia Kupitia na kutathmini hali ya usalama wa Mifumo na Miundombinu ya Serikali Mtandao na kuzishauri Taasisi za Umma katika maeneo ya kuboresha, pamoja na kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA inafanya kazi wakati wote kwa ufanisi na usalama.Pamoja na hayo Mha.Ndomba amesema kuwa Mamlaka inashirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) kwa lengo la kuhakikisha Serikali Mtandao inaimarika kote Bara na Visiwani.”Kupitia ushirikiano huu, Mifumo kadhaa imeboreshwa na inatumiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mifumo hii ni pamoja na Mfumo wa Barua Pepe Serikalini, Mfumo wa Masjala, Mfumo wa Malipo Zanzibar (ZanMalipo), Mfumo wa Ajira (ZanAjira), e-Wawakilishi na Mfumo wa Ankara za Maji (MAJIIS) kwa ajili ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA). Pia, Mamlaka inashirikiana na eGAZ katika utoaji wa huduma ya miundombinu ya Serikali mtandao,”amesema Mha.Ndomba.Aidha ameeleza kuwa Serikali Mtandao ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji kazi wa Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa wananchi. Ambapo amesema Lengo la Serikali Mtandao ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Taasisi za Umma pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa Umma ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu kupitia tehama.