November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATE wazindua Bonanza la waajiri kwa mwaka 2023

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi siku ya kilele

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bonanza la Waajiri (Waajiri Health Bonanza) kwa mwaka 2023 lenye lengo la Kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya Afya na Usalama katika maeneo ya kazi.

Bonanza hilo ambalo litaleta mjadala kuhusu umuhimu wa Afya ya Akili katika sehemu za kazi, kilele chake kitafanyika tarehe 7 Oktoba 2023 katika Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bonanza hilo la waajiri (Waajiri Health Bonanza), Mkurugenzi Mtendaji kutoka Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba amesema Bonanza hilo la ambalo limebeba kauli mbiu inayosema ‘Kuimarisha Afya ya Akili ili Kuongeza Tija Mahali pa Kazi.’ litashirikiana na
wadau wa Kazi na Ajira wakiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu-KVAU, WCF,
NSSF, PSSSF, TUCTA na OSHA katika kuandaa na kusherekea kwa pamoja katika siku zote hizo tatu za Waajiri Health Bonanza.

Amesema Bonanza hilo litaanza asubuhi kwa kufanya mazoezi ya viungo (Aerobics) kwa washiriki wote na kufuatiwa na michezo mingine kama vile mpira wa miguu (Football), Mpira wa Pete (Netball), Kuvuta kamba,Kukimbiza Kuku, Kukimbia na Magunia nk.

Pia litahusisha shughuli mbalimbali kama vile Upimaji wa Afya
utakaoambatana na ushauri kutoka kwa Wataalamu wa Afya
watakaokuwepo.

“Bonanza hili litasaidia kuhamasisha makampuni na Taasisi mbalimbali kushiriki katika kuhamasisha na kuunga mkono juhudi za kuboresha Afya ya Akili
katika maeneo yao ya kazi, Kuhamasisha Sekta binafsi kutoa kipaumbele na kushiriki katika
masuala ya Afya na Usalama, Kukuza mtandao wa kibiashara na kuongeza fursa ya kujifunza”

“Bonanza hili pia litasaidia Kuwapa Waajiri fursa ya kuhudumiwa na Wadau wetu kama NSSF,
WCF, OSHA, PSSSF pamoja na OWM lakini pia Kutoa fursa kwa washiriki kucheki afya zao na kupewa ushauri na wataalamu wa afya”

Ndomba ameziomba kampuni na Waajiri wote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki michezo mbalimbal ya Bonanza hilo.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Chama Cha wafanyakazi Tanzania TUCTA, Willy Kibona amesema suala la Afya ni kipaumbele namba moja, hivyo wanashirikiana na wadau muhimu wakiwemo OSHA, Waajiri katika sehemu mbalimbali za kazi

“Tunawaweka pamoja wale watu wa chini kuwapa elimu ili wajue faida ya kuwa na akili timamu na Afya njema, tunawahamasisha wajiunge na vyama vya wafanyakazi ili tuweze kwenda kwa pamoja, ili tufanikishe hayo lazima kuwe na Mipango madhubuti na sera mbalimbali ambazo serikali imewema pamoja na waajiri katika masuala mazima ya afya na usalama kazini”

“Kuhusu afya ya akili ni lazima uangalie kwamba ili uweze kupata tija ni lazima mfanyakazi akili yake iwe timamtu” amesema

Naye Meneja Kanda ya pwani kutoka OSHA, George Charles amesema wanafanya kaguzi mbalimbali ikiwemo kaguzi zote ambazo zinaweza kubaini kwamba mfanyakazi anaathirika kiafya

“Tunahakikishia kwamba masuala yote yanayotokana na kazi ambazo zinaweza zikasababisha msongo wa akili zinapatiwa ufumbuzi kwa kufanya maelekezo mbalimbali kwa mujibu wa sheria lakini pia Kutoa ushauri “

“Tunahakikishia kwamba wafanyakazi wanakuwa na Zile kamati za afya na usalama ambazo zinaweza zikajadili matatizo yao, inspekta anapofika kwenye maeneo ya kazi waweze kupata taarifa na kuweza kuzisimamia na kuhakikisha Yale maeneo ya kazi yana sera nzuri ambazo zinahusiana lakini pia masuala ya drug abuse ili kuzuia wafanyakazi kuzuia kutumia madawa ya kulevya na vitu vyote ambavyo vinaweza kuhatarisha afya ya akili”