January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATE wasaini mkataba wa miaka mitatu na ERB

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

CHAMA cha waajiri Tanzania (ATE) kimesaini mkataba wa makubaliano wa miaka mitatu (2024-2026) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), ambapo Bodi hiyo inaenda kuwekeza dola 39,000
kwa ajili ya wanawake 13 kushiriki katika programu ya mwanamke kiongozi.

Kupitia mkataba huo, ATE wamependekeza kila mwaka kutoa nafasi moja, ambayo Bodi hiyo haitalipia kwa muda wa miaka mitatu, ili kupeleka
wanawake wengi zaidi kushiriki katika programu hiyo.

Hayo yalisemwa na Mtendaji ATE, Suzanne
Ndomba, wakati wakizindua awamu ya 10 ya mwanamke kiongozi .

Ndomba alisema awamu hiyo ya 10 imekuwa ya utofauti kutokana na idadi ya wanawake kutoka makampuni mbalimbali 27 kushiriki kwa wingi kutoka wanawake 76 katika awamu ya 9 hadi wanawake 116 katika awamu ya 10.

Ndomba alisema lengo la programu hiyo ni
kuhakikisha kwamba wanaweza kutoa ujuzi na kuongeza ujuzi kwa wanawake kwenye masuala ya uongozi.

“Inaonesha kwamba programu hii imeweza
kuwavutia wengi na kwa sababu sisi tunadili na makampuni na jinsi gani wanawake na makampuni yanawekeza kwa wanawake kuwafanyia mafunzo
katika maeneo hayo matatu katika programu hii.

Programu ya mwanamke kiongozi inawafundisha wanawake katika maeneo matatu, umaarufu katika kuendesha vikao katika bodi , masuala ya uongozi
na mawasiliano.”

Ndomba alisema Programu hiyo itaendeshwa kwa muda wa miezi 9 kwa kuingia darasani katika vipindi vichache, lakini zaidi ya hapo watakuwa wanarudi katika maeneo yao ya kazi na kuweza
kufanya kazi kwa vitendo.

Aidha, Ndomba aliyataka makampuni mengine yaendelee kuwekeza kwa wanawake kwa kufika ATE ili wanawake hao waweze kushiriki katika programu hiyo.

“Tunafurahishwa na safari hii ya Cohort 10
kuanza na tunashawishi makampuni mengine kuwekeza kwa wanawake katika maeneo mengine tofauti na kufika ATE ili waweze kushiriki katika programu hiyo,” alisema.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Injinia Bernard Kavishe, alisema Tasnia ya uhandisi ni miongoni mwa tasnia ambazo zimekataa mfumo na katika kila wahandisi watatu
wa kiume, mmoja ni mwanamke, hivyo idadi ndogo ya wahandisi wa kike ni tatizo kwa sababu katika malengo ya maendeleo ya Dunia yanadai usawa wa kijinsia.

“Usawa wa kijinsia ukikosekana ni dalili ya
uduni wa maendeleo, hivyo tumekuwa na miradi kwa takribani miaka 20 iliyopita ya kutatua tatizo hilo kwa sababu watoto wa kiume na watoto wa kike wamekuwa na changamoto ambazo hazifanani,”alisema.

Injinia Kavishe alisema kama Bodi, kazi kubwa wanayoifanya ni kuwachagiza na kuwatia moyo watoto wakike waende na masomo hayo na baada ya kuingia katika masomo hayo inabidi walindwe na mazingira ambayo ni tofauti na watoto wa kiume.

“Watoto wa kike wanachangamoto nyingi, za kimaumbile, kitamaduni, kihistoria na kimapokeo, kwa hiyo lazima wapewe ulinzi maalumu hasa kuwekwa katika shule nzuri, ulezi mzuri mpaka watakapojiunga chuo kikuu,”alisema.

Aidha alibainisha kuwa bodi inatekeleza mradi wa miaka mitatu wa kulea wahandisi wa kike wenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 4 lengo likiwa ni kusaidia wanawake wahandisi 100 waliomaliza vyuo pamoja na kuimarisha chama cha wahandisi
wakike Injinia Kavishe alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa chachu ya kuonesha wanawake wanaweza.

Programu ya mwanamke kiongozi ni programu ambayo ilizinduliwa mwaka 2016 na Rais Samia ambapo kwa wakati ule alikuwa ni Makamu wa Rais Programu hiyo inaratibiwa na ATE na imeletwa
nchini Tanzania kupitia Umoja wa Waajiri Norway ambapo kupitia serikali yao wanatoa ushirikiano huo kwa vyama vya waajiri, lakini pia ATE na mpaka sasa program hii inafanywa Tanzania, Kenya,
Uganda, Ghana, Misiri na Jordan.