December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATCL yatoa punguzo la 5% kukata tiketi kupitia App

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) leo imezindua kampeni ya “Appy Skies” itakayowazawadia wateja wake wanaotumia “Air Tanzania App” punguzo maalumu kwenye msimu huu wa sikukuu.

Akizindua Kampeni hiyo Leo Desemba 1, 2023 jijini Dar es Salaam, Mussa Mbura, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), amesema uzinduzi wa “Air Tanzania App” ni muendelezo wa Air Tanzania katika kutumia teknolojia kwenye kutoa huduma zao.

Mbura amesema Air Tanzania App itasaidia wateja kupata huduma mbalimbali ikiwemo tiketi, mizigo na kupanga safari zao kupitia simu zao za mkononi.

“Ulimwengu wa sasa ni wa teknolojia basi huduma zao nyingi ni lazima ziendane na mahitaji ya wasafiri wa anga kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza gharama kwa wasafiri pamoja na kuongeza furaha kwa kutoa huduma za nyoongeza kwa wateja wa Air Tanzania wanapotumia App hiyo”, amesema Mbura.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mha. Ladislausi Matindi amesema pamoja na kumiliki soko la anga nchini, Kampuni ya Ndege Tanzania imeendelea kuboresha huduma zake ili kuongeza furaha kwa wadau wake haswa wasafiri na watumiaji wa huduma za ndege.

“Air Tanzania App inamleta msafiri kwenye ulimwengu halisi wa wasafiri wa anga na kumpa uzoefu wa pekee wa faragha na uhuru wa uchaguzi. Air Tanzania App sio tu kwa ajili ya kuwezesha safari bali pia inamuwezesha mteja wa Air Tanzania kunufaika na ofa za bidhaa mbalimbali. Mteja ataweza kuchagua muda wa safari, daraja la safari, kiti, kununua begi la ziada mahali popote ulipo, muda wowote anapohitaji kusafiri kwenda. sehemu yoyote ndani na nje ya nchi ambapo Air Tanzania inafanya safari zake”, amesema Mha. Matindi.

Matindi amefafanua kuwa punguzo hili ni la asilimia 5 hadi 10 ya bei halisi za tiketi, na ni kwa wateja wanaokata tiketi zao kupitia “Air Tanzania App” tu ambalo linatolewa msimu huu wa sikukuu (Holiday Bonus). Mauzo ya tiketi hizo za punguzo yameanza leo tarehe 1 Desemba 2023 hadi 1 Januari 2024.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amesema hatua iliyofikiwa ya Air Tanzania kuwa na App ya safari ni jambo la kujivunia na kufurahia kwa kila Mtanzania kwa sababu ubora wa huduma unaongezeka ambapo wananchi wataweza kufikia huduma za tiketi kwa urahisi zaidi, kupata punguzo na nyoongeza ya huduma mbalimbali zitolewazo kupitia App hiyo.

“Hili ni jambo la kujivunia, Shirika letu linakwenda kukaa katika mkao wa shughuli hizi za ndege kimataifa zaidi”, amesema Matinyi.

Kampuni ya Ndege Tanzania inatoa huduma kwenye vituo 15 vya ndani ya nchi na 11 nje ya nchi.