December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATCL yampongeza Rais.          Samia uwekezaji ATCL

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraonlineDar

KAMPUNI ya Ndege ya Air Tanzania (ATCL), imepongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua anazochukua  kuendelea kuwekeza kwenye shirika hilo hali ambayo imeliwezesha kuendelea kuhimili ushindani kwenye sokola la kitaifa na kimataifa.

Kwenye taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, shirika hilo lilisema Serikali ya awamu ya sita muda wote imekuwa ikiimarisha shirika hilo kuongeza ufanisi wake.

“Tunamshukuru Rais Samia  kwani tumeona juhudi zake za kuliinua shirika hili tangu aingie madarakani miaka mitatu iliyopita na shirika limepata nguvu ya kushindana kitaifa na kimataifa,” ilisema

Aidha, taarifa hiyo ilisema baadhi ya juhudi zinazofanywa na Serikali ni pamoja na kuendelea kununua ndege mpya za shirika na za kisasa zikiwemo za abiria na za mizigo.

Ilisema serikali imekuwa ikitoa vibali vya shirika kuajiri wataalamu wa kada mbalimbali wakiwemo marubani, wahandisi, wahudumu wa ndege na kuwezesha ufunguzi wa vituo vipya vya safari za ndege ndani na nje ya nchi.

Ilisema hali hiyo imeliwezesha shirika kutanua wigo wa mtandao wake pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu hao ili wamudu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Hivi karibuni (ATCL) ilitangaza kuwa iko kwenye maandalizi ya kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Muscat nchini Oman.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL),  Mhandisi Ladislaus Matindi,  aliyasema hayao alipokutana na Balozi wa Oman nchini, Saud bin Hilal Alshaidani tarehe 26 Juni 2024 katika Ofisi za Ubalozi zilizopo jijini Dar es Salaam.

“Taratibu za kufungua kituo nchini Oman zimeanza ambapo Air Tanzania tumeshampata wakala mkuu wa mauzo ya tiketi zake nchini Oman (General Sales Agent), tumeteua Msimamizi wa Kituo hicho” alisema Mhandisi Matindi

Aliongeza kuwa kwa sasa hatua iliyofikiwa ni kukamilisha uandaaji wa timu ya marubani, ndege itakayotumika pamoja mpangilio wa safari.

Kwa sasa Air Tanzania inafanya safari za ndani ya nchi kwa zaidi ya vituo kumi. Kwa safari za kikanda na kimataifa ina safari za Dubai (UAE), Mumbai (India), Guangzhou (China), Bujumbura (Burundi), Entebbe (Uganda), Hahaya (Comoro), Harare (Zimbabwe), Lusaka na Ndola (Zambia), Nairobi (Kenya) na Lubumbashi (Congo).

Kwa Tanzania ATCL imekuwa ikifanya safari zake kati ya Dar es salaam kwenda mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Songea, Katavi, Zanzibar, Mtwara, Tabora  na Kigoma.

Mwisho