Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WATANZANIA wametakiwa kutumia fursa ya amani na utulivu uliopo hapa nchini kwa kufanya kazi kwa bidii ili kutokomeza umaskini na baa la njaa na kujiletea maendeleo.
Wito huo umetolewa jana na Askofu Mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Jimbo la Tabora Rev.Paul Meivukie ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG-Kitete Christian Centre la mjini hapa katika ibada ya Krismasi.
Alisema Watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Mungu na kuendelea kumwomba ili amani na utulivu uliopo sasa uendelee kuwepo na kudumishwa umoja, mshikamano na kuchapa kazi kwa bidii.
Akinukuu maandiko matakatifu katika kitabu cha Wathesalonike wa 2 aya 3:10 alisema kila mtu anapaswa kufanya kazi na asiye fanyakazi asile, na kubainisha kuwa mvua zinazoendelea kunyesha sasa ni fursa muhimu sana ya kufanya kazi.
Alisisitiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhimiza watoto wao kufanya kazi ili familia zao ziwe na chakula cha kutosha na sio kuacha watoto wao kuzurura, na kubainisha kuwa hakuna sababu ya kuteseka kwa njaa.
Rev. Meivukie aliwataka waumini wa kanisa hilo na madhehebu mengine ya dini kuendelea kumwomba Mungu ili mwaka 2022 umalizike kwa amani na utulivu na awape mwaka 2023 uliojaa neema na baraka tele na usio na majanga.
Aliongeza kuwa wakiendelea kumwomba Mungu atabadilisha majira mabaya kuwa neema na baraka na lolote lililo kinyume na mapenzi yake halitatokea kamwe katika taifa letu.
Aidha Askofu Mstaafu alipongeza jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 chini ya Utawala wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha taifa linakuwa na chanzo kikubwa na cha uhakika cha umeme.
‘Tunampongeza sana Rais Samia kwa kuzindua zoezi la ujazaji maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere lililoko Rufiji Mkoani Pwani ili kuwezesha Bwawa hilo ambalo litakuwa chanzo kikuu cha umeme hapa nchini kuanza kazi’, alisema.
Aidha Rev Meivukie alipongeza hatua ya serikali kuanza kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima na kutoa bei elekezi ya mauzo yake, aliomba utaratibu wa uuzaji mbolea hiyo kuwekwa vizuri ili kuwaepushia wakulima usumbufu wanaopata.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi