Na Bakari Lulela,TimesMajira online, Dar es Salaam
MGOMBEA ubunge Jimbo la Kawe kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Askofu Josephat Gwajima ameanza kampeni za kupita nyumba kwa nyumba kwa lengo la kuomba kura kwa wananchi ambapo ameahidi wakimchagua atatatua kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa kawe jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeandaa Ilani iliyobora kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika kukabiliana na changamoto za maisha ikiwemo suala la ajira sambamba na utoaji wa mikopo kutoka halmashauri.
Akizungumza na wakazi hao jijini Dar es Salaam katika kampeni za mtaa kwa mtaa,nyumba kwa nyumba alizozifanya kwa nia ya kuomba kura kwa wakazi wa jimbo la kawe,mgombea huyo amesema CCM kupitia jemedari wake Dkt.John Magufuli kimeandaa ajira zipatazo milioni 5 hadi milioni 8 kwa lengo la kuwasaidia vijana kuondokana na tatizo la ajira.
Gwajima amesema atakapopata ridhaa ya kuongoza jimbo hilo atahakikisha anaweka miundombinu rafiki kwa wakazi wa eneo la kawe ikiwemo barabara, vituo vya afya, zahanati pamoja na kuwapatia wakazi hao maji safi na salama.
“Mtakapo nichagua nitahakikisha nazitatua changamoto zilizokuwa kero kwenu kwa kuzitafutia mwarobaini , serikali ya CCM kupitia ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani itakuwa chachu ya mabadiliko na kuhakikisha wananchi wanaishi maisha bora,” amesema askofu Gwajima
Askofu Gwajima amesema kuwa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imetenga zaidi ya sh. bilioni 2 hadi 3 kwa kipindi cha mwaka kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali kama moja ya njia ya kuwanufaisha wananchi katika uendelezaji wa shughuli mbalimbali.
Aidha Gwjima alieleza kuwa maendeleo hayana chama wala dini hivyo amewataka wakazi wa Jimbo la Kawe kuwa na imani na Askofu huyo ambae malengo yake ni kuwatumikia wananchi wa kawe kwa kuwaletea maendeleo alisisitiza umoja ni kitu cha msingi katika kupata mafanikio.
Hata hivyo mgombea huyo ameahidi kuwasaidia makundi maalumu hususani wale waliokata tamaa na maisha ambapo alisema hata katika vitabu vya Mungu vimeandika kuhusiana na jambo hilo kwa makundi hayo.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto