November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia ya waliopata Chanjo ya UVIKO-19 yaongezeka, Kishapu

Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online

BAADHI ya wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wameanza kuitikia wito wa Serikali wa kuchanja chanjo ya kinga ya ugonjwa wa Uviko-19 baada ya kubaini chanjo hiyo haina madhara kwa binadamu.

Wakizungumza na mwandishi wa Majiratimes Online mjini Mhunze Kishapu kwa nyakati na maeneo tofauti wananchi hao wamesema hivi sasa wengi wao wanajitokeza kuchanja chanjo ya uviko-19 baada ya kuwaona waliochanja hapo awali hawajapatwa na madhara yoyote.

Mmoja wa wananchi hao, Shabani Bakari mkazi wa kitongoji cha Maendeleo kilichopo mjini Mhunze wilayani Kishapu anasema awali watu wengi walishindwa kujitokeza kuchanja chanjo ya uviko kutokana na hofu ya kwamba chanjo hiyo ilikuwa na madhara.

“Ni kweli Kishapu tulikuwa nyuma katika kuchanja chanjo hii, na hii ilichangiwa na hofu ya wengi wetu kwamba ilikuwa na madhara kwa binadamu, hasa kwa sisi watu wa jinsi ya kiume, tuliaminishwa inapunguza nguvu za kiume, kumbe siyo kweli,”

“Kutokana na juhudi za viongozi wetu kutuelimisha, na kuwaona wale waliokubali kuchanja mwanzoni mpaka sasa wapo kawaida, watu wameanza kujitokeza kuchanja kwa hiari, wanaamini haina madhara kama walivyohisi hapo awali,” anaeleza Bakari.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Maendeleo mjini Mhunze, Grace Shani anasema awali wengi walihisi wakichanjwa ndiyo wanaathirika zaidi, lakini kutokana na uhamasishaji walioufanya watu wengi wameelewa na kuona umuhimu wa kuchanja chanjo hiyo.

“Dhana kwamba wanaume wakichanja wanakosa nguvu za kiume ilikuwa potofu, wala hakuna mtu aliyechanjwa kwamba akiwekewa gropu ya umeme inawaka siyo kweli, elimu tuliyoitoa kwa jamii imesaidia sana, sasa wengi wanakwenda kuchanja wao wenyewe bila kusukumwa, maana mtu aliyechanja anakuwa na tofauti kubwa na ambaye hakuchanja,” anaeleza Grace.

Baadhi ya viongozi wa kidini wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Sheikh Adamu Njiku ambaye ni Sheikh wa mtaa wa Mhunze wilayani Kishapu na Mchungaji Patrick Zengo wa kanisa la KKKT Mhunze wametoa wito kwa wakazi wa Kishapu kujitokeza kwa wingi kuchanja chanjo hiyo kwa vile haina madhara yoyote.

“Hata upande wetu sisi waislamu, mungu ametuagiza tunapopatwa na magonjwa tutumie dawa ili tupone, hakusema ombeni dua ili mpone, na akaagiza tujikinge na vitu vyovyote ambavyo vinaweza kutuletea madhara, ni wazi kuchanja chanjo ya Uviko-19 ni sehemu ya kujikinga,” anaeleza Sheikh Njiku.

Mchungaji Zengo amewapongeza watendaji wa Serikali kwa kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchanja chanjo hiyo na kwamba kwa upande wao wamekuwa wakiendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa watu kuchanja ili kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19.

“Dhana potofu ambazo zilitolewa na baadhi ya watu hapo awali ndiyo zimechangia wilaya ya yetu ya Kishapu kuwa nyuma kidogo kwa watu kujitokeza kuchanja chanjo hii ya kinga ya Uviko-19 baadhi walihisi eti mtu akichanja kisha akiwekewa balbu ya umeme inawaka, ilikuwa ni upotoshaji tu,”

“Binafsi yangu mimi natoa wito kwa watu wote wakiwemo waumini wa kanisa langu kujitokeza kwenda kuchanja, wala hakuna dhambi yoyote ya muumini kupatiwa chanjo hii, hivyo kanisa linahimiza watu kuchanja, na wajiepushe na imani potofu zinazopotosha, Serikali ina nia njema kuleta chanjo hii,” anaeleza Mchungaji Zengo.

Mratibu wa chanjo wilayani Kishapu, Jamila Mohamedi anasema hivi sasa kuna mafanikio makubwa upande wa watu kujitokeza kuchanja chanjo ya Uviko-19 ikilinganishwa na hapo awali ambapo watu wengi walikuwa na hofu juu ya chanjo hiyo na kuifanya Kishapu kuwa nyuma ki mkoa kutokana na idadi ndogo ya waliojitokeza kuchanjwa.

“Kwa sasa kuna mafanikio makubwa, mwanzoni wengi walikuwa na hofu na wengine kutokana na imani zao hasa za kimila, baadhi walihisi ukichanjwa unapunguza nguvu za kiume, mara huwezi kuzaa, lakini kadri siku zinavyokwenda wengi wameanza kuelimika,”

“Bado kuna maeneo machache sasa ambako jamii haijaona umuhimu wa kuchanja, tunapanga njia za kukutana nao ili tuweze kupata elimu, tunahisi baadhi ya watoa huduma wetu hawatimizi wajibu wao kwa kutoa elimu, tunaamini elimu ya kutosha ikitolewa wengi watachanja,” anaeleza Jamila.

Jamila amesema ugonjwa wa Uviko-19 bado upo, hivyo ni vyema kuchanja kuliko kutokuchanja na kwamba wapo watu wanaokwenda kupimwa na kuona wana maambukizi ya Uviko lakini kwa vile wamechanjwa hawaoneshi dalili zozote za kuugua ugonjwa huo.

“Huu ugonjwa bado upo na tunaishi nao lakini tutaupunguza au kuutokomeza kabisa kwa kupata chanjo maana mpaka sasa hakuna dawa unayoweza kutumia ili kutibu uviko-19, wapo watu wanapimwa hapa inaonekana wana ugonjwa, lakini kwa vile wamechanja hawaoneshi dalili zozote za kuugua, yote hii ni sababu ya chanjo,” anaeleza Jamila.

Anasema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022 wilaya ya Kishapu ilikuwa imechanja watu wapatao 123,414 kati ya walengwa 179,000 sawa na asilimia 69 ya lengo lililowekwa na kwamba kwa hivi sasa wanatarajia idadi hiyo kuongezeka baada ya elimu ya usalama wa chanjo hiyo kutolewa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya hadi kufikia Oktoba 07, 2022 palikuwa pameripotiwa visa 478 vipya vya maambukizi ya Uviko-19 nchini kote ikilinganiwa na visa 586 kwa kipindi kilichoishia Agosti 26, 2022 ikiwa vimepungua kwa asilimia 18.4 huku mkoa wa Dar es Salaam ukiendelea kuongoza kwa visa vipatavyo 382.

Hadi kufikia Oktoba 07, 2022 mikoa ya Shinyanga, Tabora, Kagera, Rukwa, Geita, Songwe, Simiyu, Njombe na Iringa hazikuwa na kesi yoyote ya wagonjwa wa Uviko-19 huku ikibainika jumla ya wagonjwa wanne waliolazwa katika kipindi hicho hawakuwa wamepatiwa chanjo ya kinga ya Uviko-19.

Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga
Mchungaji wa Kanisa la KKKT wilayani Kishapu, Patrick Zengo.
Sheikh Adamu Njuki Sheikh wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mtaa wa Mhunze wilayani Kishapu.
Grace Shani, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maendeleo mjini Mhunze, wilayani Kishapu.
Hospitali ya Wilaya ya Kishapu mkoani Kishapu.