January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 95 ya wakazi Kigoma Vijijini wapata huduma ya maji safi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kigoma

WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Kigoma Vijijini wamefanikiwa kufikisha huduma ya maji safi na salama katika jumla ya vijiji 46 kati ya 48 vilivyoko katika wilaya hiyo.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo wilayani humo Mhandisi Aron Kaje alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliotembelea wilaya hiyo hivi karibuni li kujionea utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

Amesema hadi sasa miradi 6 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika vijiji 6 na vijiji 2 vilivyobaki vitatengewa bajeti katika mwaka ujao wa fedha wa 2024/2025 ili kufikisha huduma hiyo kwa asilimia 100 katika vijiji vyote.

Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inafikishwa katika miji na vijiji vyote nchini.

Mhandisi Kaje amefafanua kuwa kwa kasi hii ya serikali ya awamu ya 6 ana uhakika azma ya kufikisha huduma hiyo kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini kama ilani ya Chama inavyoelekeza itafikiwa na kuvuka hata kabla ya mwaka 2025.

‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia zaidi ya sh bil 2 kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji miradi ya maji katika wilaya yetu kwa nyakati tofauti, tunamwahidi, miradi yote tutaitekeleza kwa weledi na ufanisi mkubwa na kwa wakati ili wananchi waendelee kuiamini serikali yao na Chama tawala’, amesema.

Aidha amebainisha kuwa chanzo cha maji cha mto Mkuti kilichoko wilayani humo kimekuwa mkombozi kwa kuwezesha wakazi zaidi ya 40,000 kupata huduma ya maji safi ya bomba baada ya kutekelezwa miradi 3 katika vijiji vya Pamira, Samwa, Kidahwe na Matendo vilivyoko katika kata za Kidahwe na Matendo na bado kina maji ya kutosha yanayoweza kunufaisha wananchi wengi zaidi kata nyingine.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa Pamira uliogharimu zaidi ya sh mil 500 na kuwanufaisha wakazi zaidi ya 16,000.

Miradi mingine ni Matendo ambao umegharimu sh bil 1.02 ambao utekelezaji wake sasa umefikia asilimia 70 na unatarajia kunufaisha zaidi ya wakazi 11 na ule wa Kidahwe unaogharimu zaidi ya mil 900 ambao sasa umefikia asilimia 96 na umeanza kunufaisha wananchi 16,200.

Matukio mbalimbali katika picha