December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 60 ya wakazi Kaliua hawana huduma ya maji safi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online. Kaliua

LICHA ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 katika kutekeleza miradi ya maji hapa nchini, asilimia 60 ya wakazi Wilayani Kaliua, Mkoani Tabora hawajapata huduma ya maji safi na salama hadi sasa.

Akizungumza na gazeti hili jana Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani humo, Mhandisi Boniface Mapambano alisema ni wakazi 230,462 tu kati ya 576,156 wanaopata huduma hiyo.

Alisema mahitaji ya maji katika wilaya hiyo ni lita za ujazo14, 403,900 kwa siku na kwa sasa wanazalisha lita 5,761,560 tu kwa siku ambapo upatikanaji huduma hiyo katika wilaya nzima umefikia asilimia 40.

Alisema wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama kwa sasa ni asilimia 40 tu ya wakazi wote 576,156 huku wakazi 345, 694 wakiwa bado hawajafikiwa na huduma hiyo.  

Mhandisi Mapambano alibainisha kipaumbele cha halmashauri hiyo katika mwaka ujao wa fedha kuwa ni kuhakikisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa wakati ili kupanua zaidi wigo wa upatikanaji huduma hiyo.

Kukamilika kwa miradi hiyo inayogharimu zaidi ya sh bil 4.5 na itakayotekelezwa katika mwaka ujao wa fedha 2023/2024 kutaongeza upatikanaji huduma ya maji safi katika jamii kutoka asilimia 40 ya sasa hadi asilimia 69 ifikapo Juni 30, 2024.

Alifafanua kuwa wilaya hiyo yenye tarafa 5, kata 28, vijiji 99 na vitongoji 458 hadi sasa ina vituo vya kuchotea maji (dp’s) 558 katika maeneo mbalimbali, ambapo vinavyofanya kazi ni 365 na 193 havifanyi kazi kutokana na sababu mbalimbali.

Alitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni kuharibika pampu na visima kukauka maji, na kubainisha kuwa zoezi la ukarabati visima hivyo linaendelea ikiwemo usanifu wa miradi mipya na kukamilisha inayoendelea kutekelezwa.

Mhandisi Mapambano alibainisha kuwa katika mwaka ujao wa fedha wanatarajia kutumia zaidi ya sh bil 2 kwa ajili kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kukamilisha ambayo haijakamilika ili kuongeza upatikanaji huduma hiyo.

Baadhi ya miradi itakayotekelezwa ni uchimbaji visima vipya na ukarabati visima visivyofanya kazi kwa kubadilisha vipuri, upanuzi na ujenzi wa miradi mipya, utafiti wa maji chini ya ardhi na usanifu wa bwawa la maji kijiji cha Zugimlole.

Wananchi wakichota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji (dp’s) vilivyojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Kaliua Mkoani Tabora . Picha na Allan Vicent.