January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 10 ya watu wanaoishi Duniani wana ugonjwa sugu wa figo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Asilimia 10 ya watu duniani wanaishi na magonjwa sugu ya figo huku asilimia 50 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 75 wana ugonjwa sugu wa Figo.

Hayo yamesemwa na Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe wakati wa ufunguzi wa kongamano la kisayansi la wauguzi wataalamu wa Africa lililofanyika jijini Dar es Salaam.

“Dhima ya kongamano hili ni kuleta maendeleo ya huduma ya magonjwa ya figo Duniani ambapo jukumu la elimu na ubunifu kwenye nchi za Afrika na dhima hii imekuja kwa wakati muafaka ambapo Tanzania inaenda kuimarisha na kupanua upatikanaji wa huduma za figo”. Amesema Dkt. Sichalwe

Dkt. Sichalwe amebainisha kuwa Mpaka Janauri 31, 2022 wagonjwa 2750 nchini Tanzania kwa sasa ndio wanapata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na kufikia tarehe 31 Januari mwaka huu wagonjwa 325 wamepandikizwa Figo.

Pia, Kati yao wagonjwa 93 wamepandikizwa nchini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa 67 na Hospital ya Benjamin Mkapa Dodoma 26.

Aidha Dkt. Sichalwe amesema kwasasa hospitali zinazotoa huduma ya kusafisha damu nchini ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali zote za Rufaa za Kanda (Bugando, KCMC, Benjamin Mkapa, Mbeya na muhimbili) na hospitali za Rufaa za Mikoa ya Kagera, Mwanza, Musoma, Kigoma, Arusha, Iringa na Mtwara.

“Ni matumaini yangu kuwa kongamano hili litatusaidia kujua hali halisi ya ugonja huu, changamoto tunazokutana nazo katika kutoa huduma za afya ya figo na njia za kuweza kukabiliana nayo”. Amesema Dkt. Sichalwe

Hata hivyo Dkt. Sichalwe amesema Pamoja na kuimarisha huduma za magonjwa ya figo katika nchi zetu, Wauguzi lazima kujipanga kuweka jitihada za kipekee ili kupambana na ugonjwa huu hatari kwa kuimarisha afya za kinga kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Kongamano hilo linafanyika kwa siku mbili ikiwa limehudhuriwa na idadi ya nchi tisa za Afrika ikiwepo nchi ya Kenya, Uganda, Misri, Rwanda, Sudani ya kusini, Burundi, Ghana, Zambia na wenyeji Tanzania.

Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Aifelo Sichalwe akifungua zawadi aliyokabidhiwa na muuguzi mkuu kitengo cha vyama vya wauguzi wa nefonolojia afrika Dkt. Divina Nyirera kutoka nchini Kenya