Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,amesitisha kwa muda wa mwezi mmoja(siku 30), utoaji wa mikopo wa asilimia 10, kwa makundi ya wanawake,vijana na walemavu inayotolewa na Halmashauri.
Hiyo ni kwa Halmashauri zote zilizopo ndani ya Mkoa wa Mwanza baada ya kubaini takribani asilimia 56 ya fedha za mikopo zilizokopeshwa kwa makundi hayo kwa miaka mitatu kutorejeshwa kwa wakati na kubaini mapungufu katika utoaji wa mikopo hiyo ambayo ni kinyume na kanuni ya utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019.
Mhandisi Gabriel, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Mwanza, ambapo amesema mikopo iliotolewa kwa kipindi cha 2018-2021 ni zaidi ya bilioni 8.7 huku mikopo ambayo haijarejeshwa ni zaidi ya bilioni 4.9.
Amesema kumeku na vikundi vilivyokopeshwa tangu 2018-2021 kutorejesha kwa wakati mpaka Februari mwaka huu,lakini ni kinyume na ya kanuni ya utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ya mwaka 2019 kanuni ya 10 namba (1,2).
“Nasikitika tunakaribia mwezi wa tano tangu mwezi wa pili 2022 tunadai zaidi ya bilioni 4.9 lakini sijapata taarifa kamili ya vikundi kama vimepatiwa notisi fedha ambazo hazijarejeshwa ni sawa na asilimia 56 zaidi ya nusu ya fedha zote hazijarejeshwa katika kipindi hiki kifupi cha utoaji mikopo,kuanzia leo ndani ya siku 30 naomba nisimamishe utoaji wa mikopo kwenye halmashauri zote kwa lengo la elimu kuanza kutolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni na kupata vikundi sahihi,” amesema Mhandisi Gabriel.
Amesema,mikopo hiyo siyo zawadi bali inatolewa kwa vikundi vya kina mama,vijana na walemavu ili waweze kutumia na kujiinua kiuchumi na baadae warejeshe ili na vikundi vingine viweze kukopeshwa kila kikundi ambacho kimepata mkopo chini ya kanuni hizo wanatakiwa kurejesha mkopo baada miezi mitatu tangu siku ambayo kilipata mkopo.
Pia ameeleza kuwa kumekuwa na ukiukwaji wa Kanuni za utoaji na usimamiaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hivyo wote waliohusika kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa huku akiziomba timu za Mkoa waone namna ya kusaidia fedha hizo zinakuwa salama maana ni fedha nyingi na zinarudishwa na kosa hilo lisirudie tena.
Amesema Kamati yake ya utafiti imefanya kazi katika Halmashauri zote na kubaini changamoto kwenye maeneo mbalimbali juu ya utoaji wa mikopo hiyo ambapo kuna Halmashauri ambazo zilitoa mikopo kwa vikundi ambavyo vilikuwa havijasajiliwa lakini wameona katika Halmashauri mbili takribani milioni 800 zimetolewa kwa vikundi ambavyo havijasajiliwa.
Changamoto nyingine ni uwepo wa wana vikundi wenye ajira rasmi waliopewa mikopo kinyume na kanuni ya 6 sehemu ya kwanza kifungu kidogo F, ambacho kinasema kikundi hakutajumlisha wajumbe wenye ajira rasmi.
Ambapo kumekuwepo na watumishi na watu wenye ajira ambao wamepokea kiasi cha zaidi ya milioni 59,ambapo inawezekana wenye kikundi labda walijificha wakasema wanastahili lakini kutokana na wakaguzi na timu za wasimamizi yakabainika hayo.
Hivyo wito wake kwa watumishi wote na watu wenye ajira kwenye vikundi vyote walivyokopeshwa wajitokeze katika halmashauri ambazo wamepewa hizo fedha na kukutana na uongozi wa Wilaya na Halmashauri wawe na utaratibu wa ndani wa namna nzuri kuona fedha hizo zinarejeshwa.
Pia kulitolewa mikopo kwa vikundi bila ya kuwa na utambulisho wa vikundi kutoka kwa watendaji wa Kijiji,Mitaa na vitambulisho vya wajasiriamali kwa wakati huo, ambapo kanuni namba 7 sehemu ya 3(b) kifungu kidogo inasema kuambatanisha nakala halisi ya nyaraka zifuatavyo barua kutoka kwa Mtendaji wa Kijiji au Mtaa kwa kadri itakavyo kuwa na Mtendaji wa Kata.
Ambapo wameona kuna mikopo imetolewa kuanzia mwaka 2019 yenye jumla ya zaidi ya bilioni 1.2. ambayo imetolewa kwa vikundi ambavyo havikuwa na utambulisho wa vikundi kutoka kwa watendaji yani mtu hajulikani ni nani,yupo wapi.
Kuwepo kwa vikundi kukosa uthibitisho wa kuwa fedha za mikopo zilizotolewa zilitumika kama kusudio la mradi au andiko la mradi.
Aidha ameeleza kuwa changamoto kubwa ilijitokeza katika ufuatiliaji ni kuwa na utoaji wa mikopo hiyo pasipo kutoa tangazo kwa umma la utoaji wa mikopo kinyume na kanuni jambo linaloathiri suala la uwazi na kupelekea utoaji wa mikopo kwa upendeleo na kutokuwepo kwa utawala bora.
“Kama Mkuu wa Mkoa natangaza kulinda,kuheshimu,kuenzi suala la utawala bora,unaozingatia kanuni na sheria zinazotuongoza katika mambo mbalimbali ikiwemo jambo hili,hivyo basi jumla ya mikopo iliyotolewa bila ya kufuata kanuni hii ni zaidi ya bilioni 3.4,hivyo wote waliohusika wahakikishe fedha hizo zinarejeshwa na marejesho yanapatikana ili vijana wengine waweze kunufaika,” amesema.
Vile vile ameeleza kuwa na vikundi ambavyo vilipata mkopo vikiwa havijamaliza mkopo wa awali ambapo ni kinyume na kanuni ambapo kiasi cha zaidi ya milioni 73.1 vikundi vimepokea fedha hivyo ameagiza waliochukua fedha hizo warejeshe.
Sanjari na hayo pia kumekuwa na changamoto ya utoaji wa mikopo yenye thamani ya zaidi ya milioni 635 kwa vikundi 138 ambavyo maombi hayakupitishwa kwenye vikao vya kisheria timu ya menejementi,wala kuhidhinishwa na Kamati ya fedha,mipango na uongozi wala kupitishwa na Baraza la Madiwani na wote waliohusika kuhidhisha fedha hizo wazifuatilie.
Vikundi 59 havikuwa na katiba ya kikundi lakini walipewa mikopo na wanaendelea kufuatilia huku katika tume aliounda vikundi 94 vilivyotembelewa na kuchunguzwa ilibainika vikundi 30 vilivyo orodheshwa kwenye rejesta havipo kabisa,viliisha sambaratika na wanakikundi hawajulikani walipo.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote