Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga
JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia kijana aitwaye Paschal Msindo(21) mkazi wa Kijiji cha Kalepula wilaya ya Kalambo kwa tuhuma za kumuua baba yake kwa kumkata shoka shingoni.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa, Shadrack Masija, akitoa taarifa ya tukio hilo jana alisema kuwa lilitokea Octoba 29 majira ya saa 7 mchana ambapo kijana huyo alimkata shoka shingoni baba yake mzazi aitwaye January Msindo(83) na kumuua papo hapo.
Amesema kuwa kabla ya tukio hilo mzee Msindo alikuwa amechota maji kwaajili ya matumizi ya nyumbani ambapo alikua akiyafuata umbali mrefu kutokana na changamoto ya ukame kwani visima vingi vimekauka kijijini hapo.
Kamanda Masija amesema kuwa baada ya mzee huyo kuchota maji ndipo kijana wake alitaka kuchukua maji hayo kwaajili ya matumizi yake ndipo baba yake alipo mkatalia na kumtaka akachote na yeye maji yake, ndipo kijana huyo alipo kasirika.
Baada ya kijana huyo kukasirika aliingia ndani na kuchukua shoka Kisha kumvamia baba yake na kumkata mara mbili shingoni na kumsababishia jeraha kubwa lililovuja damu nyingi na kufariki dunia muda mfupi kabla hata ya kupatiwa matibabu.
Kamanda huyo amesema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kufanya mauaji hayo alikimbilia porini lakini polisi walianza msako baada ya taarifa kutolewa kituoni na walifanikiwa kumkamata akiwa amejificha huko.
Amesema kuwa anashikiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji hayo muda wowote kuanzia Sasa mara tu upelelezi wa awali utakapo kamilika.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024