Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Dar
JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kupitia madiwani wa halmashauri nchi nzima, wamejipanga kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mafanikio hayo ni miradi ya maendeleo kwenye sekta, idara na taasisi mbalimbali ikiwemo huduma za jamii kama maji, elimu, afya, umeme na barabara. Lakini pia na maboresho mbalimbali ikiwemo stahiki za watumishi, kuongeza watumishi ikiwemo watendaji wa vijiji na mitaa.

Hayo yamesemwa leo Machi 19, 2025 na Mwenyekiti wa ALAT Taifa Murshid Ngeze wakati anazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli ameleta fedha nyingi za maendeleo kwenye mamlaka zetu, tumetekeleza miradi mikubwa kwenye mamlaka zetu. Sasa hiyo miradi, hayo mambo, twende kuyasemea kwa wananchi, twende kuwaambia, na Rais Dkt. Samia alitolea mfano, usipojisemea, hakuna atakaekusemea. Kwa hiyo ni lazima twende kusema, na hapa ni lazima nitoe wito kama Kiongozi wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa.
“Ni wakati sasa kwa madiwani nchi nzima, kila diwani kwenye kata yake kuanza kufanya mikutano ya hadhara, kila kitongoji, kila kijiji na kila mtaa, na kwenye makundi ili kuwaeleza wananchi yale yote mema yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, jinsi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilivyotekelezwa kwenye maeneo yao”amesema Ngeze.
Ngeze amesema yapo mengi yaliyotekelezwa na Rais Dkt. Samia, kwa yale yanayoonekana na yale yasiyoonekana. Na kuongeza kuwa miundombinu ya majengo ya zahanati, vituo vya afya na hospitali. Pia miradi ya maji, miundombinu ya barabara, madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, hayo yoye yanaonekana, lakini kuna mengine ameyafanya, lakini hayaonekani kwa wananchi wa kawaida, hivyo yote hayo wakayaelezee.

“Yapo mambo yanaonekana, mfano vyoo vinaonekana, madarasa yanaonekana, majengo ya zahanati, vituo vya afya, na hospitali, barabara za lami zinaonekana. Lakini kuna mambo hayaonekani mfano ajira. Mimi nawapa mfano, Rais Samia anaingia madarakani mwaka 2021 tulikuwa na uhaba mkubwa wa watendaji wa vijiji na mitaa. Natolea mfano Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, sisi tuna vijiji 94, anaingia madarakani tulikuwa na upungufu wa watendaji 40, lakini leo hii, hakuna kijiji hakina mtendaji wa kijiji.
“Tulikuwa na upungufu mkubwa wa walimu, lakini walimu wameajiriwa, tulikuwa na upungufu wa wahudumu wa afya, lakini nao wameajiriwa. Mpaka sasa hivi wameenda mbali, wanataka kuajiri mhudumu wa afya kila kijiji ili sasa kwenye jamii ile husika kuwepo na mtu ambaye amepewa mafunzo ya afya ili pale ambapo kuna upungufu wa Nurse (Muuguzi) aweze kusaidia”amesema Ngeze.
Ngeze amesema yapo mengine ameyafanya, lakini yanajulikana kwa wachache kama kuwapandisha madaraja watumishi, kuhimiza kusimamia sheria, taratibu na miongozo, ambapo mtendaji akikosea, hata yeye anafuata taratibu za kumchukulia hatua mtu huyo, huku akieleza hata kipato cha mtu mmoja mmoja kimeongezeka.
“Watu wanaweza kusema hayo yote kama vyumba vya madarasa, miundombinu ya zahanati, vituo vya afya na barabara kuwa yote tunayaona, lakini vipi kipato cha mtu mmoja mmoja. Nataka kusema, hata mapato ya mtu mmoja mmoja yameongezeka. Mfano, halmashauri ilikuwa ina masoko, lakini yale masoko yameboreshwa, na kuboreshwa kwa soko kunagusa kipato cha mtu mmoja mmoja.

“Twende kwenye kilimo, miradi ya BBT (Kujenga Kesho iliyo Bora) unaona inavyofanya kazi, unaona masoko yanavyofanya kazi na kutoa fursa kwa wananchi. Sasa hivi magari yanakwenda vijiji kuchukua mazao. Nitoe mfano, wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani, kilo moja ya kahawa ilikuwa sh. 2,100 hadi 2,500, lakini sasa hivi kilo moja ya kahawa inakwenda hadi sh. 6,000 au sh. 5,500. Hayo ndiyo mambo tunatakiwa tuyatangaze kwa wananchi” amesema Ngeze.
Ngeze ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Rukoma, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, alisema wanatekeleza maelekezo aliyoyatoa Rais Dkt. Samia wakati anafungua Mkutano Mkuu wa 39 wa ALAT Taifa ikiwemo ukusanyaji wa mapato yanayotokana na Mapato ya Ndani. Lakini pia kutaka mapato hayo yaweze kukusamywa na kuwekwa kwenye Mfuko wa Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya wananchi, badala ya wajanja wachache kutumia.
“Suala la ukusanyaji mapato, Rais Dkt. Samia alilisisitiza sana. Kwanza alifurahi sababu halmashauri zimeongeza ukusanyaji wa mapato, lakini akahimiza tuendelee kuongeza umakini katika ukusanyaji huo wa mapato, lakini pia tuendelee kubana matumizi ili sasa yale tunayofanikiwa kuyakusanya zaidi, tuweze kuyawekeza kwenye miradi ya maendeleo ambayo yanasaidia wananchi kwenye mamlaka zetu.
“Lakini jambo la pili ambalo alilihimiza na kulielekeza, ni kuendelea kuweka mipango yetu ya halmashauri kwa kuendana na mipango ya maendeleo yetu ya nchi ya Dira ya Taifa 2025- 2050. Kwamba, mipango yote tunayopanga kwenye halmashauri, iendane na Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Kwa hiyo sasa ni wakati wa halmashauri kwenda kuangalia mipango yetu kama inaendana na Mpango wa Maendeleo 2025- 2050.
“Lakini jambo la tatu ambalo alilielekeza, twende kubuni vyanzo vipya vya halmashauri. Lengo la Serikali ni kuona halmashauri zianze kujitegemea kwenye mamlaka zetu, na ziache kuitegemea Serikali Kuu, na ndiyo maana unaona Rais Dkt. Samia anahimiza tuendelee kubuni vyanzo vya mapato, na tuweze kuwa na mapato ya kutosha na kuweza kujitegemea, na jambo la nne alilosisitiza ni kusimamia sheria kwenye halmashauri zetu” amesema Ngeze.

Ngeze ametaja Maazimio ya Mkutano Mkuu wa 39 wa ALAT Taifa kuwa wananchi wahamasishwe ili washiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025; majibu ya maombi ya halmashauri kuruhusiwa kufanya matengenezo ya magari na mitambo katika karakana za halmashauri yafuatiliwe katika mamlaka husika ili kupunguza gharama kubwa zinazotozwa na TEMESA.
Madeni ya ada za Uanachama.
Ada za uanachama za mwaka zikatwe moja kwa moja kutoka mapato ya ndani,kila halmashauri iingize deni la michango ya ada ya uanachama kwenye vitabu vya mahesabu za Halmashauri (Financial statement), kila mwaka wa fedha halmashauri zipunguze madeni, yaani kila robo mwaka kwa asilimia tano ya deni hivyo kwa mwaka mzima halmashauri itakuwa imelipa deni kwa asilimia 20.
Kamati ya Utendaji ya ALAT – Taifa iweke mikakati ya kuhakikisha madeni yote ya michango ya ada ya uanachama yanalipwa kwa wakati. Udanganyifu wa risiti za malipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu na Halmashauri ya Jiji la Mbeya:- Halmashauri ziwachukulie hatua za kinidhamu watumishi wote waliohusika na kuthibitika kushiriki katika tuhuma za katika kutengeneza risiti za malipo zisizo halali kwa malipo watuhumiwa wote kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na taarifa zioneshwe katika vyombo vya habari na kuwasilishwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na mamlaka zingine zinazohusika na tuhuma za udanganyifu wa risiti za malipo.
ALAT ihakikishe inahuisha maadhimisho ya Wiki ya Serikali za Mitaa nchini,Halmashauri ihakikishe inaendelea kuimarisha mifumo inaendelea kusomana ili kurahisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mpato;, halmashauri kujizatiti katika dhana ya ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato kujiimarisha na kuweza kupunguza utegemezi rasilimali kutoka Serikali Kuu;

More Stories
NACTVET yawahakikishia wadau, usimamizi thabiti wa ubora wa elimu ya Ufundi na Amali
Wasira awataka Wenyeviti CCM kuiga mfano Mkoa wa Mbeya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,yajizatiti kuboresha uwezo wa Mawakili wa Serikali