October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ajali yaua mawakala wanne CHADEMA

Na Israel Mwaisaka,TimesMajira Online, Sumbawanga

WATU wanne ambao ni mawakala wa kusimamia Uchaguzi Mkuu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamefariki dunia papo hapo baada ya kupinduka na gari lenye namba za usajili T.381 BZQ aina ya Noah.

Tukio hilo lilitokea jana saa 02:00 asubuhi katika Kijiji cha Malonje, Kata ya Mollo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wakisafirishwa kutoka katika mji mdogo wa Laela kwa lengo la kwenda kula kiapo.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Justin Masejo amesema, tukio hilo lilitokea baada ya gari kumshinda dereva aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Aswile aliyekuwa akiendesha gari hilo kwa mwendo kasi mkubwa.

Kutokana na mwendo huo, dereva alishindwa kulimudu gari hilo ambalo liliacha njia na kwenda kugonga gema la barabara na kisha kupinduka.

Kamanda Masejo amesema kuwa, baada ya gari hilo kupinduka, mawakala wanne walifariki dunia papo hapo, huku wengine wakijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kutunzia maiti katika hospitali ya Mkoa wa Rukwa ili ndugu zao wafike kuitambua na majina yao bado hayajafahamika.