December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aiomba Serikali kumpa ajira za kushona sare za Polisi,JKT

Na Penina Malundo ,Timesmajira

MUHITIMU kutoka Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) Songea,Riziki Ndumba,ameiomba serikali kuweza kumpa ajira ya kuweza kushona sare za Jeshi la Polisi au Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili aweze kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika maonesho ya 48 ya Biashara kimataifa Sabasaba Ndumba ambaye ni mlemavu wa mkono, amesema tangu ahitimu mwaka 2021 bado hajaweza kujiajiri kutokana na kutokuwa na mtaji hivyo anaiomba serikali iweze kumsaidia.

“Kujiajiri mwenyewe naweza changamoto ni mtaji,lakini kama nitapata ajira nitashukuru zaidi hata kwenye taasisi ya Jeshi la Polisi au Jeshi la Kujenga Taifa nikajihusishe na mimi angalau kushona sare zao uwezo huo mimi ninao.

“Naiomba serikali iweze kunipa ajira kama ina uwezo huo, kama iliweza kuniamini ikanipokea VETA pamoja na ulemavu wangu, nina imani serikali yangu ni sikivu haiwezi kuacha kunipa ajira,” amesema.

Hata hivyo ameishukuru VETA kwa kuweza kumpa ujuzi huo pamoja na kuiomba jamii isiweze kuwaficha wenye ulemavu kwani wakiwezeshwa wanaweza.

“Nilikuwa sina ujuzi wowote lakini baada ya kufika VETA nimekuwa fundi ambaye naweza kushona nguo ya aina yoyote. Napenda niiase jamii kuwa hakuna kitu ambacho kinashindikana mimi leo hii ni mlemavu wa viungo lakini nilipokwenda kusoma VETA walinipokea vizuri wakanipa ushirikiano na hatimaye leo hii nimeweza kuwa fundi mzuri.

“Kama upo mtaani au kuna mtu yoyote mwenye changamoto ya ulemavu kama mimi mlete VETA wala msimfiche kwasababu ukifika utakutana na viongozi wenye uwezo wa kutambua huyu mwenye changamoto hii tumuweke kwenye fani gani, watakuchagulia fani inayoendana na wewe,” amesema na kuongezwa:

“Napenda kuishukuru serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya pamoja na kuwekeza katika shule za ufundi stadi,ambapo na sisi tumepata fursa kusoma “.