January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ahadi ya Rais Samia kwa TAHLISO yatimia


*Serikali yazindua Mwongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa stashahada, yatenga sh. bilioni 48, dirisha kufunguliwa Ijumaa

Na Irene Clemence, TimesMajira Online

AHADI ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwapatia mikopo wanafunzi wa vyuo vinavyotoa elimu kwa ngazi ya stashahada nchini, imetimia baada ya Serikali kuzindua mwongozo wa utoaji wa mikopo ya elimu.

Uamuzi huo wa Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi hao unafuatia ombi lililotolewa kwa Rais Samia na viongozi wa  Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (TAHLISO) walipokuna naye, Ikulu, jijini Dodoma.

Baada ya ombi hilo, Rais Samia aliahidi kulifanyia kazi na kutoa maelekezo kwa Waziri wa Elimu kuangalia namna ya kufanya kwenye bajeti yake.

Mikopo hiyo inaanza kutolewa kwa wanafunzi hao kwa mwaka wa masomo 2023/2024, ambapo Serikali imeainisha maeneo sita ya wanufaika wa mikopo hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa utoaji mikopo hiyo  Jijini Dar es Salaam jana katika Ofisi za Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojioa, Profesa Adolf Mkenda, alisema utoaji wa mikopo hiyo ni dhamira ya serikali kuona vijana wengi zaidi wa kitanzania wanapata elimu na ujuzi ili kushiriki katika ujenzi na maendeleo ya Taifa.

Pia alisema HESLB imefungua dirisha la maombi kwa njia ya mtandao kwa siku 15 kuanzia  Oktoba 7 hadi Oktoba 22,mwaka huu.

Alisisitiza kwamba watakaofanikiwa kwa kupata mkopo wasichezee  fedha hizo, badala yake wajikite katika masomo ili kukidhi malengo ya Serikali katika maeneo yenye uhitaji hususani kwa kupata walimu wa masomo ya hisabati na fizikia.

Alisema Serikali kupitia sekta ya elimu ilifanya tathmini na kuainisha maeneo sita kulingana na mahitaji ya soko baada ya kubainika kuwa na uhitaji wa wataalamu.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni afya na sayansi shirikishi, ualimu( masomo ya fizikia, hisabati na mafunzo ya amali), usafiri na usafirishaji, uhandisi na nishati, madini na sayansi ya ardhi na kilimo na mifugo.

“ Serikali ilifanya tathmini ya uhitaji wa wataalamu katika  nchi yetu na kubaini maeneo hayo yana uhitaji mkubwa wa wataalamu  katika ngazi ya kati kwa sababu serikali imejenga na kukarabati shule, ambazo zinahitaji walimu wa sayansi na pia inatekeleza  mageuzi makubwa kwa sekta ya mafuta, gesi, madini na kilimo,” alisema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda alisema kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024, wanafunzi takribani 8,000 watakaodahiliwa kusoma stashahada katika fani mbalimbali wanakaribishwa kuomba mikopo.

Alifafanua kuwa Serikali imetenga sh. bilioni 48 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi hao.

“Ni dhamira ya Serikali kuona vijana wengi wananufaika  na elimu na ujuzi ili kushiriki katika ujenzi na maendeleo ya taifa na dhamira hiyo imedhihirishwa kutokana na ongezeko la bajeti ya fedha za mikopo kufikia sh. bilioni 731 kwa mwaka 2023-2024, kuanzishwa kwa fursa ya Samia Scholaship kwa wastani wa wanafunzi 640,” alisema.

Aidha aliwataka waombaji wa mikopo  kufuata utaratibu, kwani Mwongozo wa utoaji mikopo utaanza kupatikana kwa lugha ya Kiswahili katika tovuti ya Wizara ya Elimu.

Baada ya kumaliza masomo, mwanafunzi mnufaika atapaswa kurejesha mkopo kwa kiwango cha asilimia 15 kutoka katika mshahara wake wa mwezi.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi ya HESLB, Prof Hamisi Dihenga alisema imefika wakati jambo hilo limefanikiwa baada ya kuwepo maswali mengi kwa watu.

Alisema baada ya uzinduzi wa mpango huo kazi kubwa iliyobakia ni kuendelea kutoa elimu kwa umma waweze kuelewa masharti ya vitu gani ambavyo vinahitajika ili waweze kupata mkopo .

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Adolfu Rutayunga alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kukamilisha adhma hiyo kwani ilikuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.

“Wanafunzi wanaosoma stashahada wakipata mikopo itaongeza idadi ya wanaotaka kusoma katika fani hizo,  kwani takwimu nchini zinaonesha watu walio na shahada ni wengi kuliko stashahada, hivyo sio vizuri kwa sababu utendaji kazi unahitaji kuwepo na mchanganyiko,” alisema.

Naye, Rais wa  Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu(TAHLISO), Maria John, alimshukuru Rais Samia  kufanikisha utekelezaji wa suala hilo.

Alisema uamuzi huo utaleta hamasa kwa wanafunzi wengi kusoma fani hizo na kukidhi mahitaji ya soko.

“Tunakumbuka tulipowasilisha ombi letu katika kikao chetu na Rais Samia mkoani Dodoma, alilipokea kwa unyenyekevu mkubwa na leo kalifanikisha, hivyo tunawaomba wanafunzi husika wakaombe kwa kuzingatia vigezo vilivyoelekezwa,” alisema John.