November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afya Kwanza yachunguza 260 saratani ya matiti, tezi dume

Na Mwandiishi wetu, TimesMajira Online,Mwanza

WATU 260 jijini hapa wamejitokeza ili kuchunguzwa saratani ya matiti, shingo ya kizazi na tezi dume ambapo 72 kati yao wameonesha viashiria vya kuwa na moja ya maradhi hayo.Uchunguzi huo umefanyika chini ya mradi maalumu wa Afya Kwanza Tanzania chibni ya mashirika saba yasiyo ya kiserikali hapa nchini .

”Walioonesha viashiria vya magonjwa hayo ni wanaume 29 na wanawake 43 na wote tumewarufaa kwa uchunguzi zaidi katika hospitali za wilaya na Bugando. Wale watakaothibitika rasmi tutasimamia matibabu yao katika hospitali za serikali,” alisema Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Nseya Kipilyango.

Sababu za kuendesha mradi huo jijini hapa, alisema ni tafiti za kisayansi kuonesha kwamba wagonjwa wengi wa saratani wanatoka katika Kanda ya Ziwa.

“Tumeendesha zoezi la upimaji bure kwa kila aliyefika. Uchunguzi wetu ulijikita zaidi katika kuchunguza viashiria vya awali vya magonjwa hayo,” alisesema Mhandisi Kipilyango.

Alitaja idadi ya waliopimwa kila aina ya saratani pamoja nawalioonesha viashiria kwenye mabano ni tezi dume 298 (15), shingo ya kizazi 378 (32) na matiti 380 (13).

Katika watu walioonesha viashiria, alisema wengi wao ni wazee wasio na watu wa karibu wa kuwasaidia jambo ambalo litawafanya wahitaji nguvu ya ziada kuwasaidia.

“Mradi wetu haukujiandaa kutoa msaada wa kuwatunza. Hili ni jambo litakalohitaji kuomba ufadhili wa ziada,” alisema Mhandisi Kipilyango.

Isitoshe, alisema walijitokeza watu wengi kiasi kwamba ilibidi waombe msaada wa wahudumu wa afya kutoka zahanati na hospitali jirani lakini hawakufanikiwa kuwahudumia wote.

Alimshukuru Mbunge wa Buchosa wilayani Sengerema, Eric Shigongo kwa kuwaongoza wakazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi.

Alisema lengo la Afya Kwanza ni kutoa huduma ya upimaji katika kanda yote ya Ziwa lakini hiyo itategemea na iwapo wafadhili watawezesha mpango huo.

Mhudumu wa Afya Kwanza akielimisha wakazi wa Buchosa wilayani Sengerema, Mwanza kuhusu umuhimu wa kufanyiwauchunguzi wa saratani mbalimbali