December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afisa Mtendaji Wazo huru achangia madawati 20 shule ya msingi Kiomboi-Bomani

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Singida

AFISA Mtendaji Mkuu wa kampuni ya WazoHuru Media Mathias Canal amechangia madawati 20 katika shule ya msingi Kiomboi-Bomani iliyopo Wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida.

Mathias amechangia madawati hayo Mei 2024 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinaimarishwa na kuhakikisha kuwa sekta ya elimu nchini inaendelea kuimarika.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi na walimu wa shule hiyo wakiongozwa na Mkuu wa shule Mwalimu Sadick Mkoma wamemshukuru Mathias kwa kujitoa kwake kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wazazi pamoja na serikali.

 Canal amesema kuwa serikali inafanya kazi kubwa kwa ajili ya kuijenga nchi hivyo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo elimu wadau wanapaswa kushiriki kuchangia ili kuimarisha sekta mbalimbali kuunga mkono juhudi za serikali.

“Msingi wa maisha na mafanikio madogo niliyonayo ulianzia Shule ya msingi Kiomboi Bomani, wazazi wangu pamoja na wazazi wa hawa watoto wanaosoma Kiomboi Bomani wamenilea na kunivumilia kwa kila namna hivyo njia pekee ya kuwashukuru ni kuwafanya watoto wao wakae kwenye madawati sio chini,”

“Wakati mwingine tunaweza kuwalaumu wanafunzi kwa utoro au matokeo mabovu darasani lakini kumbe tatizo ni mazingira magumu wanayopitia darasani ikiwemo kukaa chini,”amesema Canal

Canal amesema kuwa amepata wazo hilo la kutoa madawati kutoka na kuona jitihada za serikali  kuweka miundombinu mizuri ikiwemo ujenzi wa madarasa, imeajiri walimu wa kutosha, hivyo wadau nao wanapaswa kuungana na serikali kwa hali na mali.