November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afisa Elimu Dar aipongeza St. Mary’s kwa nidhamu na taaaluma

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,online,Dar

AFISA Elimu wa Mafunzo ya Walimu Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam,Tungalaze Mkembi, ameimwagia sifa shule ya St Mary’s Mbezi kwa ubora wa taaluma na nidhamu kwa wanafunzi wake.

Ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya 21 ya shule ya St Mary’s Mbezi yaliyofanyika Mbezi jijini Dar es Salaam, ambapo alisema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma na alishauri wazazi wa wahitimu wa darasa la saba kuwapeleka watoto wao kwenye shule ya sekondari St Mary’s.

Mkurugenzi Mwenza wa Shule za St Mary’s Tibe Rwakatare akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa darasa la saba wa shule ya St Mary’s Mbezi jijini Dar es Salaam, Farhan Abdulaziz, wakati wa mahafali ya 21 ya shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo. Kushoto ni Afisa Elimu wa Mafunzo kwa walimu Manispaa ya Kinondoni, Tungalaze Mkembi

Amesema mbali na kufanya vizuri kitaaluma wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakilelewa kwenye maadili mema na aliwashukuru walimu kwa namna ambavyo wamekuwa wakifundisha kwa weledi na kupata matokeo mazuri.

“Nasisitiza wahitimu tuendelee kusoma St Mary’s kwasababu ni shule ambayo tumeizoea na kitaalumaa kwa Manispaa ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa shule ambazo tunajivunia kwa kweli,” amesema

Wanafunzi wa shule ya st Mary’s Mbezi jijini Dar es Salaam, wakikata keki kwaajili ya kuwalisha wazazi kwenye mahafali ya 21 yaliyfanyika shuleni hapo na kuhudhuriwa na wazazi na walezi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mwenza wa shule za St Mary’s Tibe Rwakatare alisema shule hiyo inajivunia matokeo mazuri ya kitaaluma inayopata kila mwaka na imejigamba kuwa kisiwa cha nidhamu kutokana na namna inavyowalea wanafunzi wake kwenye maadili mema.

Amesema shule hiyo imejitahidi sana kuweka mazingira mazuri sana ya nidhamu kwa wanafunzi wake na imeendelea kufanya vizuri kitaaluma kulinganisha na siku za nyuma.

Ametoa mfano kuwa kwa upande wa shule ya sekondari wamefanya vizuri zaidi kwani kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka jana wanafunzi wa shule hiyo walifaulu kwa kiwango kikubwa .

Wahitimu wa darasa la saba wa shule ya St Mary’s Mbezijijini Dar es Salaam, wakionyesha vyeti vyao vya kuhitimu wakati wa mahafali ya 21 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo.

“Kwa mliokuwepo kwenye mahafali ya mwaka jana niliwaambia matokeo yatakuwa mazuri na kweli yalipotoka mlijionea wenyewe maana tulipata daraja la kwanza 15 na 28 daraja la pili na daraja la tatu 34 na kidato cha pili 19 walipata daraja la kwanza, 10 daraja pili na daraja la tatu 11,” alisema

Amewashukuru walimu na wafanyakazi wa shule hiyo kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana katika ufundishaji ili kuhakikisha anapata mafanikio ya kitaaluma na kwamba wanafunzi hao wanaomaliza darasa la saba wameiva vya kutosha.

Mmoja wa wahitimu waliofanya vizuri wa darasa la saba shule hiyo, Farhan Abdulaziz akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa shule hiyo, Tibe Rwakatare mwenye suti nyeusi na mgeni rasmi kushoto wakati wa mahafali yaliyofanyika shuleni hapo

Amesema anatarajia matokeo mazuri kwa wanafunzi hao kwenye mitihani ya mwisho ya darasa la saba inayoratajiwa kufanyika Septemba 8 na 9 mwaka huu kutokana na namna walivyofundishwa na walimu mahiri na waliobobea.