November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AFCA kuongeza thamani ya Kahawa Nchini

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

CHAMA cha Kahawa Bora za Afrika (AFCA) kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) wamesema Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Maonyesho ya 21 ya Kahawa Bora za Afrika (AFCC&E) mwaka 2025 ambalo linatoa fursa ya kuonyesha ubora wa kipekee wa kahawa za Afrika kwenye jukwaa la kimataifa.

Tukio hilo linatarajiwa kufanyika februari 26-28, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa JNICC jijini Dar es Salaam ambapo itakuwa ni fursa kwa watanzania kuonesha umuhimu wa Tanzania katika sekta ya kahawa.

AFCC&E ni jukwaa kubwa zaidi la biashara ya kahawa barani Afrika litawakutanisha zaidi ya wadau 2,000 kutoka ndani na nje ya bara pamoja wazalishaji wa kahawa, wafanyabiashara, wakaangaji na wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa serikali ili kujadili na kukuza ukuaji na ushirikiano katika sekta ya kahawa.

Kauli mbiu ya Kongamano la 21 la AFCC&E ni “Kuhuisha Ongezeko la Thamani,” na litakuwa na orodha ya wazungumzaji maarufu kimataifa na kikanda, Kongamano hilo pia litajumuisha maonyesho yatakayoonyesha ubunifu na maendeleo ya hivi karibuni katika sekta ya kahawa na warsha, vipindi vya kuonja kahawa (B2B cupping sessions) na ziara maalum zilizopangwa kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu kahawa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Primus Kimaryo, amesisitiza umuhimu wa tukio hilo kwa wakulima wa ndani kuwa ni fursa ya kipekee kwa wakulima kuboresha ubora wa kahawa zao Kwa kuzingatia kuwa bei ya kahawa kwa sasa ni nzuri duniani na ni fursa ya kupanua wigo wa masoko.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Kahawa Bora za Afrika (AFCA) Amir Hamza, ameeleza manufaa mapana zaidi kwa kubainisha kuwa, Fursa iliyopo kwa wadau wa kahawa ni kuleta kahawa zetu na kuzionyesha kwa dunia, Kila mmoja anayeshughulika na kahawa atakuwepo, kuanzia watengenezaji wa mitambo hadi wanaoongeza thamani, wanaozalisha vifaa vya kufungashia na zaidi Watanzania watanufaika kiuchumi kwa njia nyingi lakini hasa wadau wa kahawa.

Kongamano hilo pia litajumuisha Mashindano ya watayarisha kahawa Afrika na Mashindano ya kahawa bora katika ukanda wa Afrika ambayo yataonyesha vipaji bora na bidhaa za kahawa bora kutoka kote barani Afrika.