November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ado:Wafanyabiashara wa soko la Manzese B wanatakiwa kushirikishwa uvunjwaji wa soko lao

Na Mwandishi wetu, timesmajira, Online

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kusitisha mpango wa kuvunja Soko la Manzese B lililopo Manispaa ya Songea hadi wafanyabiashara wa soko hilo wataposhirikishwa vya kutosha na kulipwa fidia.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo alipokwenda sokoni hapo jana na kufanya Kikao na wafanyabiashara wa soko hilo.

“Nimeambiwa Serikali inataka kuvunja soko hili na kujenga soko jipya la Kisasa. Hatua hiyo ni njema. Lakini ninafahamu soko hili lilijengwa na nyinyi wafanyabiashara na Mkataba wenu na Halmashauri unamalizika Mwaka 2025. Hivyo basi si haki kwa Serikali kutaka kulivunja kabla ya kuzungumza na nyinyi na kuwalipa fidia”-Amesema Ado.

“Nimeelezwa kuwa mmepewa notisi ya kuhama ifikapo tarehe 1 Julai, 2022. Ninamuomba Waziri Mwenye dhamana ya TAMISEMI Ndugu Innocent Bashungwa kuingilia suala hili. Mradi huu hauwezi kutekelezwa kabla ya kuwalipa fidia wafanyabiashara na kuwatafutia maeneo mazuri ya kwenda. Pia, mradi ukikamilika, wafanyabiashara wa sasa wapewe kipaumbele kupewa maeneo”,amesema Ado.

Ado ametoa wito pia kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwamulika Wawakilishi wake wa ngazi za chini kwa sababu baadhi ya maamuzi yao yanawaumiza Wananchi masikini na hivyo kuipaka matope Serikali.

“Soko hili lina wafanyabiashara 700. Unapowaumiza watu 700 unakuwa umeumiza maelfu ya familia zao na kuwajengea chuki na Serikali”,amesema Ado.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha Serikali za Vijiji zinazingatia taratibu za uuzaji wa ardhi ya kijiji

Ado ametoa rai hiyo alipotembelea Kijiji cha Kipingo kilichopo Jimbo la Madaba mapema jana tarehe 16 Juni 2022. Wananchi wa Kijiji hicho walimlalamikia Ndugu Ado juu ya kitendo cha Serikali ya Kijiji kuuza zaidi ya hekari 1500 za Kijiji bila baraka za Mkutano Mkuu wa Kijiji. Wanakijiji hao wanadai wale ambao wamekuwa wakihoji dhidi ya suala hilo wamekamatwa na Polisi, kupigwa na kubambikiwa kesi.

Ado amewaahidi Wanakijiji hao kuwa Chama cha ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta watalifuatilia suala hilo.