October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ADC:Tukamalize hasira kwa kupiga kura na sio kuvuruga amani ya nchi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Iringa

“WATANZANIA tulinde amani yetu, hivyo Oktoba 28 tukamalize hasira zetu kwenye masunduku ya kupiga kura na sio kuvuruga amani ya nchi”

Hiyo ni kauli ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama ADC,Queen Cuthbert Sendiga alipokuwa akizungumza na wakazi wa Iringa Mjini eneo la kituo cha zamani wakati akiomba kura.

Amesema kuwa ili amani iliyopo nchini haipaswi kuchezewa na kama Watanzania wana hasira ni vyema hasira hiyo wakaimaliza kwa kupiga kura na si kuchezea amani.

“Amani yetu haipaswi kuchezewa kabisa ni vyema kama mna hasira mkaimaliza kwa kupiga kura na si kuivuruga kwani Tanzania ni nchi ya amani na itaendelea kuwa na amani,” amesema.

Amesema kuwa Mkoa wa Iringa ni kati ya mkoa uliobarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba na hali ya hewa ya kurutubisha mazao ya biashara kama nyanya,vitungui,mahindi na mbogamboga ni Iringa.

Amesema kuwa imefika wakati sasa wananchi wakaichagua ADC ili iwaletee maendeleo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto za wakulima ambao wamekuwa wakizalisha lakini kutokana na ukosefu wa soko la uhakika mazao hayo yamekuwa yakiharibikia shambani.

“Mazao yanayozalishwa yanaonekana mengi shambani lakini kwa ukosefu wa masoko yamekuwa yakioza shambani ninawaomba muichague ADC ili iwaletee maendeleo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto hizi.

“Watanzania wakitupatia ridhaa ya kuongoza nchi hii ifikapo Oktoba 28 tunakwenda kujenga viwanda vya kutosha kulingana na uzalishaji uliopo mkoani hapa ili kuongeza tija kwa wakulima na ajira kwa wana Iringa,” amesema.

Mh Queen pia ameomba wananchi wa Jimbo la Iringa mjini kumchagua mgombea Ubunge wa ADC Daudi Issa Masasi ili aweze kutekeleza Ilani ya chama cha ADC ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto walizonazo ambazo kwa muda mrefu zimekosa ufumbuzi. 

Mgombea huyo wa urais Queen anaendelea na ziara yake ya lala salama katika Mkoa wa Singida.