December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ADC watoa ombi kwa Rais Samia

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online-Tanga

KATIBU Mkuu wa Chama cha Alliance Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Serikali inapitia upya na kuziangalia tena kesi za uhujumu uchumi, utakatishaji wa fedha na kesi za ugaidi ambazo zinawakabili baadhi ya watanzania wanaoteseka magerezani kwa muda mrefu.

Hatua hiyo ya Katibu mkuu huyo inatokana na namna ambavyo Rais Samia alivyoonesha dhamira ya kupambana haki na wajibu, hivyo kumuomba aangalie vizuri sheria na ziweze kufanyiwa marekebisho lakini pia waliokamatwa na kuwekwa magerezani Serikali iangalie namna ya kuzifuta kesi hizo ili watanzania waweze kushiriki katika juhudi za kulijenga Taifa.

Katibu Mkuu huyo amesema, kutokana na kesi za uhujumu uchumi, utakatishaji wa fedha na kesi za ugaidi kutokuwa na dhamana inapelekea wengi kuendelea kuteseka.

Amesema, kwa sababu Rais ameonyesha dhamira ya kupambana na kesi za namna hiyo basi ziangaliwe upya na ziweze kufutwa.

“Watanzania wenzetu wanaendelea kuteseka na kesi hizo ambazo hazina dhamana kwa sababu Rais ameonyesha nia ya kupambana basi aangalie namna ya kubadilisha hizi sheria zinazowakandamiza watanzania wenzetu, kwa nini tunatoa ushauri huu, kwa sababu tumemsikia Rais mwenyewe akisema kwamba Takukuru wamefuta kesi zaidi ya 140 za kubambikiza,”amesema.