Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga
HAKIMU wa mahakama ya mwanzo Kasanga iliyopo wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, Michael Royan(31) anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu katika nyumba ya kulala wageni ya Safari Bar iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoani Rukwa, Theopista Mallya alisema juzi kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 27 majira ya saa 5 asubuhi baada ya marehemu kutoamka kutoka kwenye chumba alichokua amelala katika nyumba hiyo ya kulala wageni.
Alisema kuwa asubuhi ya siku hiyo ofisa upelelezi wa mkoa wa Rukwa alipigiwa simu na mtu anayeitwa Benard Wilfred ambaye alijitambulisha kuwa ni mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni na kueleza kuwa katika nyumba yake ya kulala wageni kuna mteja ambaye amelala na hajaamka na inaonekana kuwa amepoteza fahamu.
Baada ya Polisi kufika eneo hilo waliingia ndani ya chumba hicho na kumchukua mtu huyo kisha kumkimbiza hospital ya Rufani ya mkoa ya Sumbawanga ambapo alipokelewa na baada ya uchunguzi wa awali wa kitabibu ilibainika kuwa mtu huyo tayari amefariki dunia.
Kamanda Mallya alisema kuwa Polisi walipo anza uchunguzi wa tukio hilo walibaini kuwa marehemu alikua ni mtumishi wa serikali katika idara ya mahakama Mkoani katika mahakama ya mwanzo na kituo chake lilikuwa ni Mahakama ya mwanzo Kasanga.
Pia Alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda marehemu alikunywa sumu, lakini baadhi ya viungo vyake vya mwili vimechukuliwa na kupeleka sampuli kwa mkemia mkuu ili kupata majibu sahihi ya nini kilicho sababisha kifo cha Hakimu huyo.
Kamanda huyo alisema kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote hivyo imekua ni vigumi kufahamu sababu za tukio hilo lakini alisema kuwa jeshi la Polisi kinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na litatoa taarifa baada ya uchunguzi huo kukamilika.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu