“Chama cha ADA – TADEA kikiwa na ridhaa ya umma ya kuunda Serikali kitasimamia malengo ya mpango wa maendeleo ya Taifa, na nikiwa Rais wa Tanzania nitahakikisha nasimamia utawala bora wa demokrasia ya vyama vingi ya kuwa na siasa na uongozi bora wenye ushirika wa elimu ya uraia,” |
Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online.Shinyanga
CHAMA cha African Democratic Alliance (ADA-TADEA) kimeahidi iwapo kitapewa ridhaa ya kuunda Serikali moja ya vipaumbele vyake itakuwa ni kusimamia demokrasia ya Vyama vingi na Utawala bora.
Ahadi hiyo imetolewa na mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, John Shibuda kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za kunadi Sera na Ilani ya uchaguzi ya ADA – TADEA uliofanyika wilayani Maswa mkoa wa Simiyu.
Shibuda alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania moja ya mambo atakayoyapa kipaumbele ni suala la kuimarisha demokrasia ya vyama vingi na utawala bora pamoja na kusimamia ndoto za Taifa ambazo ni Uhuru na Kujitegemea na Uhuru ni kazi.
Alisema serikali ya ADA TADEA itasimamia utekelezaji wa malengo ya mpango wa maendeleo ya taifa ikiwemo kuhakikisha Tanzania inakuwa na siasa na uongozi bora wenye ushirika wa elimu ya uraia.
Hata hivyo alisema yapo mambo ambayo Rais Dkt. John Magufuli ameyafanya anayostahili kupongezwa na sasa anapaswa kupumzika na kumkabidhi yeye usukani wa Urais akiamini atakuja pongezwa kama ambavyo hivi sasa anavyopongezwa Rais Dkt. Magufuli.
“Chama cha ADA – TADEA kikiwa na ridhaa ya umma ya kuunda Serikali kitasimamia malengo ya mpango wa maendeleo ya Taifa, na nikiwa Rais wa Tanzania nitahakikisha nasimamia utawala bora wa demokrasia ya vyama vingi ya kuwa na siasa na uongozi bora wenye ushirika wa elimu ya uraia,”
“Mukthadha wa Chama cha ADA – TADEA ni kusimamia utawala wa matumizi ya mamlaka ya kisiasa, kiuchumi na vinginevyo katika kusimamia masuala ya nchi ya ngazi zote ikiwemo siasa bora, pia nitakuwa na uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji wa watu, ufanisi, tija uadilifu na matumizi sahihi ya dola,” Shibuda.
Pia mgombea huyo amewaomba watanzania kuhakikisha wanaendelea kuilinda hali ya amani iliyopo hivi sasa hapa nchini ambapo amesema iwapo itatoweka itakuwa ni vigumu kuirejesha tena huku akisisitiza kuepukwa kwa wale wenye malengo ya kuichafua wakidai “Liwalo na liwe potelea mbali.”
Hata hivyo mgombea huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Muungano wa vyama vya siasa hapa nchini ameviomba vyama vyote vya siasa kuacha kutumia maneno yenye ukakasi kwenye kampeni zao ambayo yanaweza kuwa chanzo cha kutoweka kwa hali ya amani na utulivu uliopo hapa nchini.
Katika hatua nyingine mgombea huyo amewanadi wagombea udiwani na ubunge kwa tiketi ya Chama cha ADA TADEA wanaogombea nafasi hizo kwenye majimbo ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi mkoani Simiyu ambapo amewaomba wakazi wa majimbo hayo kutumia kura zao vizuri kwa kuwachagua wagombea wa chama chake.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani