December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Act Wazalendo wapongeza Halmashauri Kuu ya CCM kuhusu mchakato wa Katiba Mpya

Na Mwandishi Wetu,timesmajira,Online

CHAMA cha ACT Wazalendo Kimeipongeza Chama cha Mapinduzi CCM ,kwa taarifa iliyotolewa baada ya kumalizika Kikao Cha Halmashauri Kuu kilichofanyika jana Dodoma na kupitisha uamuzi wa kuishauri Serikali kufufua na kukamilisha mchakakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo na Katibu wa Habari, Uenezi, Mahusiano na Umma Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo,Salim Bimani, amesema wanapongeza hatua hiyo kubwa sana.” Mwenyekiti wa Taifa wa Chama chetu Juma Duni Haji amefarijika kuwa mazungumzo yake na Viongozi Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar yamezingatiwa katika Uamuzi huu,”amesema

Amesema faraja yao inatokana na ukweli kuwa mazungumzo waliyoyasukuma na kuyaenzi yameanza kuonyesha matunda.

Hata hivyo amesema , Chama Chao cha ACT Wazalendo kimependa kusisitiza kuwa Mchakato wa Upatikanaji wa Katiba Mpya uzingatie maoni ya Watanzania waliyoyatowa na kuratibiwa na Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba (Tume ya Warioba).

Amesema wametambua kuwa ni lazima kuwepo na mchakato wa kupata mwafaka wa namna ya kufanikisha mchakato wa Katiba mpya hivyo wao , tayari wameshawasilisha Mapendekezo yao kwa Kikosi Kazi Cha Rais wa Samia Suluhu Hassan.

“Tunaamini kuwa Kikosi Kazi kitaratibu maoni na mapendekezo ya Vyama vyote na wadau wengine na kuyafikisha Serikalini ili mchakato wa Katiba mpya uanze ifikapo Mwezi Oktoba kama tulivyopendekeza,”amesema na kuongeza

“Tunatarajia juhudi za kukamilisha Mchakato wa Kupata Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi zitakwenda Sambamba na kuharakisha Mchakato wa Maridhiano ya Zanzibar,”amesema