November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT Wazalendo na CUF wajitoa kwenye uchaguzi mdogo wa marudio

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online Tanga

Chama cha ACT wazalendo jijini Tanga kimejitoa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani katika kata ya Mnyanjani kwa madai kuwa Mawakala wa Chama hicho kuzuiliwa kuingia vituoni mbali na kuwa na sifa, Kuapishwa na kupatiwa fomu za uthibitisho wa Uwakala wao katika vituo 22 na kukataa kutoa uthibitisho kwa Mawakala 7 walioapa huku wakisema ACT Wazalendo haitatambua Matokeo maovu ya Uchaguzi huo.

Vyama vilivyojitoa kwenye uchaguzi huo mdogo wa udiwani ni pamoja na chama cha ACT Wazalendo na CUF.

Awali akitoa msimamo wa chama hicho Mbarala Maharagande ambaye ni
Msimamizi wa Uchaguzi ACT Kata ya Mnyanjani jijini Tanga amesema kuwa Pamoja na jitihada mbalimbali zilizochukulia kupatia ufumbuzi suala kuanzia ngazi ya Taifa mpaka Kata, Wasimamizi wameshindwa kushughulikia kwa Wakati na wameonyesha nia ovu katika Uchaguzi huo.

Maharagande amesema kuwa Chama kimefikia uamuzi wa kuwaondoa Mawakala wake wote katika vituo vichache walioruhusiwa kuingia vituoni na hivyo kuwaondoa mawakala wote 29 vituoni na kuwaachia CCM waendelee na Uchaguzi wao wa kupanga kwa kadri watakavyoona inafaa.

Aidha, Chama kinawataka Wanachama wake, wapenzi na Wananchi kwa Ujumla waendelee na shughuli zao wasikubali kupoteza muda wao kushiriki katika uchaguzi huo.

“Uchafuzi wa Uchaguzi huu unadhihirisha uhalali na ulazima wa Madai ya ACT Wazalendo ya kupatikana kwa Tume huru ya Uchaguzi nchini mapema iwezekanavyo wananchi wamepoteza Imani na Kauli zisizotafsiriwa kivitendo na Rais Samia za kutaka kuleta demokrasia ya kweli Nchini, “alisisitiza Maharagande.

Aidha amesema anasikitishwa na Tume ya Uchaguzi kushindwa kushughulikia Changamoto zilizoripotiwa kwa wakati na kuonekana wazi wakiwa sehemu ya njama na hila zilizopangwa kuharibu Uchaguzi kwa maslahi ya CCM.

“Uharibifu huo wa Uchaguzi umeliofanyika ni pamoja na Mawakala 7 Kati ya 29 kutokupewa fomu za uthibitisho wa Uwakala wao, Wasimamizi wa Uchaguzi kuwazuia Mawakala wenye fomu za uthibitisho kuingia vituoni kufanya kazi zao kwa kutoorodhesha majina yao katika vituo husika pamoja na kukuta mabox ya kura yakiwa yamejazwa Kura ‘Fake’ muda mfupi Baada ya kuanza zoezi la kupiga kura saa 1 kamili asubuhi, “alisema Maharagande.

Amesema jambo jingine lililoharibu uchaguzi huo ni pamoja na orodha ya wapiga kura kutofautiana na iliyotolewa na NEC na wapiga kura halali kuondolewa, kutokuwepo katika daftari la Kurasa za Wapiga kura Kukosekana na kutolea mfano Kituo Cha Kwanjeka Shule ya msingi na mpangilio wa vifaa kuwekwa katika vituo hauonyeshi Uwazi, Haki, Uhuru wa Uchaguzi.

Akizungumza na kituo hiki aliyekuwa Mgombea udiwani wa kata hiyo Thobias Haule amesema kuwa wananchi na wapiga kura wamekosa haki yao ya msingi ya kumchagua kiongozi wao wanayemtaka jambo ambalo linakosesha uhuru wa demokrasia.

“Wananchi wangu poleni sana mtu ambaye mlikuwa mnamtaka awe diwani wenu ndio hivyo tena na ambaye hakutakiwa kuwa diwani wenu ndio huyo anakwenda kuwa diwani, kwanza kabisa nimepoteza rasilimali fedha, muda na rasilimali watu ndio maana tukaamua tukae pembeni tuwaachie zoezi lao, “alibainisha Haule.

Naye Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa Hamad Kidege amesema kuwa wapinzani wanapodai tume huru ya uchaguzi maana yake wanataka watu wa tume ya uchaguzi wasiwe waajiriwa wa serikali kwenye kazi nyingine na kushauri watu wa tume ya uchaguzi wakatafutwe nje ya watumishi wa serikali ili ilete tija na wananchi wafanye uchaguzi wa haki na kumchagua mwenye sifa stahiki katika jamii yao.

“Tumeingia kwenye uchaguzi huu kama kipimo cha kupima kama kweli Rais mama Samia anahitaji demokrasia ya kweli kulingana na mazungumzo yake anayozungumza na vyama vya siasa kwahiyo sisi uchaguzi huu tunautazama kama kipimo sisi kama viongozi lakini wananchi pia wanatazama kama kipimo cha ukuaji demokrasia, “alisema Kidege.

MSIMAMO WA CHAMA CHA WANACHI CUF JIJINI TANGA.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwemyekiti wa CUF wilaya ya Tanga Hamis Mnyeto amesema kuwa chama hicho kimeamua kujiondoa kwenye mchakato huo kutokana na mawakala wao kuzuiliwa kuingia kwenye kusimamia uchaguzi licha ya kupata kiapo huku masanduku ya kura yakionekana yamejaa muda mfupi tu mara baaada ya kuanza mchajato huo.

Msimamizi Mkuu wa uchaguzi jimbo la Tanga ambaye ni Mkurugenzi wa jiji la Tanga Sporah Liana amesema hali ni shwari na mchakato umeenda vizuri isipokuwa mgombea wa chama cha wananchi CUF aliwatoa mawakala wake akidai kwamba masanduku yamejaa ikiwa ni muda mfupi tu mara baada ya kuanza mchakato huo.

“Wakati huo ilikuwa kama saa moja na nusu wanasema sanduku tayari lina kura 15 anasema ni mapema eti muda huo box kuwa na kura hizo nikawaza tu kwamba wamehesabuje hizo kura ndani na zipo chini na kujua ni 15 sijui lakini niliwaambia kwamba mkiwatoa sababu mawakala wengine bado wanaendelea na tayari huyu alishaingia akasema hapana ngoja niwatoe mawakala wangu, “alisema Liana.