Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Kiongozi mstaafu wa ACT Wazaledo, Zitto Kabwe amesema endapo chama hicho kitaongoza halmashauri ya wilaya ya Buhigwe baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kitahakikisha kinalipa thamani zao la muhogo ili kuwainua kiuchumi wakulima wa zao hilo.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni jana, Oktoba 09, 2025 katika kata ya Nyamugali, jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Zitto alisema chama chake kitaondoa watu wa kati katika biashara ya zao hilo na kuwaunganisha wakulima na wenye viwanda katika nchi za Burudi na Rwanda.
Zitto amefafanua kuwa kwa sasa bei ya zao hilo katika majimbo ya Kakonko, Kasulu vijijini na jimbo la Buhigwe ni kati ya shilingi 100 hadi 200 kwa kilo, wakati katika nchi za Burundi na Rwanda bei ya kilo ya mihogo ni shilingi 2,467 inapouzwa viwandani.
“Sera yetu sisi ACT Wazalendo kwa mujibu wa ilani ya chama chetu ni kuondoa hawa watu wa kati, tutaweka utaratibu ambao umoja wa wakulima wataingia mkataba moja kwa moja na viwanda vinavyonunua mihogo na mtauza kwa shilingi 700 hadi 1000 kwa kilo”, amesema Zitto
Aidha amesema chama chake kitaandaa mazingira yatakayoruhusu kujengwa kwa viwanda katika mkoa wa Kigoma vinavyozalisha bidhaa zitokanazo na mihogo ili kuongeza thamani ya zao hilo nchini na kutengeneza fursa za ajira.

Naye mgombe ubunge wa jimbo la Buhigwe, Frank Ruhasha amesema anagombea jimbo hilo ili kupambana kuondoa changamoto za uraia zinazowakabili wananchi wa eneo hilo.

Frank amesema akiwa na miaka 11 alishuhudia maafisa wa uhamiaji na askari polisi wakimkamata mzazi wake na kumpiga wakimtuhumu sio raia wa Tanzania, jambo ambalo lilimsukuma kusoma kwa bidii ili siku moja aje atatue changamoto hiyo.

More Stories
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10