January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Acheni kutoa taarifa za uongo kwa viongozi’

Na Kija Elias,Timesmajira Online. Siha

WANANCHI wametakiwa kuacha kutoa taarifa za uongo kwa viongozi wa serikali pindi wanapotembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Mhandisi Emmy George alitoa baada ya wananchi wa Kijiji cha Munge kumweleza Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Mollel kuwa mradi wa maji uliozinduliwa Machi 16 mwaka huu haujawahi kutoa maji.

Akiwa kwenye ziara yake jimboni humo kukagua miradi ya maendeleo Mbunge wa Jimbo la Siha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ametembelea mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 600.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wananchi wa Kijiji cha Munge, wameulalamikia mradi huo tangu uzinduliwe kwenye wiki ya maji iliyoanza Machi 16 mwaka huu, haujawahi kutoa maji na kuwaomba viongozi wanaohusika na mradi huo kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Hata hivyo baada ya malalamiko hayo kutolewa na wananchi, Kamati ya Bodi za Maji Lawate-Fuka, Losaa Kia na Kamati ya Maji ya Kijiji walifanya ziara ya kukagua vilula vyote, ili kujiridhisha kama maji hayo kweli hayatoki jambo ambalo wamebaini halina ukweli wowote.

Akizungumza Wakala anayehusika na kuuza maji katika kilula ambacho kilitolewa malalamiko hayo, Diana Paulo amesema maji hayo hayajawahi kukatika hata siku moja kuanzia mradi huo uzinduliwe.

Akikabidhi mradi wa maji wa Losaa Kia, Mhandisi George amesema jukumu la RUWASA ni kujenga miradi na kukabidhi kwa bodi, ambazo zina vyombo vya watumiaji kwa ajili ya uendeshaji.

Amesema mradi huo umetekelezwa na Mkandarasi Mbesso Construction Co.Ltd kwa gharama ya sh. 643,791,244.12 ambao kwa sasa unahudumia wananchi 3,809.