March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas, Xiaomi washirikiana kuimarisha huduma za Kidigitali kwa Watanzania

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

KATIKA kuimarisha upatikanaji wa huduma za kidijitali, Kampuni ya Mawasiliano nchini, Yas, imeingia kwenye ushirikiano wa kimkakati na Xiaomi, Kampuni inayoongoza kwa ubunifu wa kiteknolojia duniani.

Kampuni hizo zimezindua simu janja Redmi 15C kwenye soko la Tanzania – hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa simu janja na huduma za kidigitali kote nchini.

Kupitia ushirikiano huu, wateja wa Yas watanufaika na simu yenye uwezo mkubwa na bei nafuu, iliyoundwa kuendana na maisha ya kidijitali.

Redmi 15C itauzwa kwa Tsh 310,000 ikiwa imeambatanishwa na GB 78 za bure kutoka Yas, zenye muda wa matumizi wa mwaka mzima – hatua inayohakikisha mteja anafurahia huduma mbalimbali mtandaoni, bila hofu ya kumaliza bando.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Yas, Ikunda Ngowi anayehusika na Vijana na Wateja wa Kati, amesisitiza umuhimu wa ubia huo.

“Upatikanaji wa mtandao wa uhakika umekuwa muhimu zaidi, na hii ni fursa kubwa kwetu.

“Kupitia ushirikiano na Xiaomi, tunawapa wateja wetu zaidi ya simu – tunawapa uzoefu bora unaorahisisha utiririshaji wa maudhui, intaneti yenye kasi, na mawasiliano bila usumbufu.

“Hatua hii inaonyesha dhamira ya Yas katika kukuza ujumuishi wa kidijitali na kuwawezesha Watanzania kuunganishwa na huduma za uhakika,” amesema Ikunda Ngowi.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Xiaomi, Eric Mkomoye amesema Ushirikiano wao na Yas unaonyesha dhamira yao ya pamoja ya kuhakikisha teknolojia ya kisasa inapatikana kwa kila mtanzania.

Amesema, Redmi 15C imetengenezwa kukidhi matakwa ya soko la sasa ikiwa na Muundo mwembamba wa kisasa wenye mvuto kwa vijana. Uwezo mkuwbwa wa kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja, kutazama video na michezo mbalimbali.

Ikiwa imeunganishwa na mtandao wa kuaminika wa Yas, qanawapatia wateja uzoefu wa kidijitali unaoendana na maisha na matarajio yao.

”Ushirikiano wa Yas na Xiaomi unaakisi mwelekeo unaokua barani Afrika ambapo waendeshaji wa mawasiliano wanashirikiana na chapa kubwa za teknolojia duniani ili kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali.

“Kwa kuzingatia ongezeko kubwa la matumizi ya simu janja na intaneti nchini, ubia huu unatarajiwa kuwawezesha zaidi vijana na kundi la wateja wa kati kubaki wakiunganishwa bila mikwamo na kufurahia burudani mtandaoni,” amesema.

#