Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wananchi wa Korogwe cha muda mrefu cha kutaka kujengewa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Old Korogwe- Magoma- Mashewa- Maramba hadi Mabokweni kilomita 128.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 30, 2025 mjini Korogwe, Dkt. Samia amesema barabara nyingine itakayojengwa kwa kiwango cha lami ni ile ya kutoka Soni- Bumbuli- Dindira- Kwashemshi hadi Old Korogwe kilomita 74.

“Kwa upande wa miundombinu ya barabara, tunakwenda kuifungua Korogwe kwa barabara za kiwango cha lami. Na kama ilivyo kwenye Ilani ya Uchaguzi, njia tutakayoenda kuanza nayo ni ile barabara ya Soni- Bumbuli- Dindira- Old Korogwe. Na barabara ya Old Korogwe- Kwamndolwa- Magoma- Mashewa- Bombo Mtoni- Mabokweni yenye kilomita 128 itajengwa kwa lami” amesema Dkt. Samia.
Dkt.Samia amesema ili kuufungua kiuchumi Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Korogwe, mipango ya kujenga Bandari Kavu kule Old Korogwe ipo pale pale, lakini pia reli kutoka Tanga hadi Musoma ikipitia Moshi na Arusha itajengwa yenye urefu wa takribani kilomita 1,108.
Mgombea ubunge Jimbo la Korogwe Mjini kwa tiketi ya CCM CPA Charles Njama alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kupeleka fedha nyingi za maendeleo kwenye jimbo hilo.

“Watu wa Korogwe, Mama tunakushukuru kwa namna ulivyotekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Umeweza kutuletea sh. bilioni 28 kwa ajili ya Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji Kata ya Kwamndolwa, na sasa tunakwenda kutekeleza Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji Kata ya Kwamsisi. Mradi huu unakwenda kuongeza kipato kwa watu, kuongeza upatikanaji wa chakula, na kuboresha hali ya watu wa Korogwe.
“Pia umetuletea sh. bilioni 24.5 kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara, na mmoja wapo wa mradi mkubwa wa barabara unaokwenda kuanza ni huu wa kutoka hapa kwenda Hospitali ya Magunga, na barabara ya Mtonga- Mgombezi hadi Bagamoyo. Mradi huu unakwenda kuutengeneza Mji wa Korogwe, na kwenda kupendeza zaidi. Ni barabara za lami zinazokwenda kuwekwa taa za barabarani na mifereji, na haya yote yanafanyika kutokana na uthabiti mzuri wa Mama Samia Suluhu Hassan”amesema CPA Njama.

Njama alimueleza Dkt. Samia kuwa Mji wa Korogwe ulikuwa na changamoto kubwa ya maji, lakini tatizo hilo linakwenda kumalizika kutoka na miradi mikubwa ya maji ukiwemo ule wa Miji 28 na Mradi wa Maji chanzo cha Mto Ndemaha.
“Wilaya ya Korogwe na Jimbo letu la Korogwe Mjini tumekuwa na changamoto ya maji ya muda mrefu, lakini sasa tuna uwezo wa kutembea kifua mbele kwa kusema changamoto hii inakwenda kuisha. Tumepata Mradi wa Maji wa Miji 28, na mradi huu unakwenda kuongeza upatikanaji wa maji na kuwa lita milioni 10.8 (kwa siku), wakati kwa sasa mahitaji yetu ni lita milioni 6.3 (kwa siku). Tukichanganya na vyanzo vyote vya maji yanayokwenda kuzalishwa ni lita milioni 16.7, hivyo tunabakiwa na ziada ya lita milioni 10.4, hivyo inatuhakikishia kuwa na uhakika wa maji kwa miaka 25 hadi 50 mbele.
“Kwenye elimu umetusaidia kuwalipia ada watoto wetu wa shule za msingi na sekondari sh. bilioni 6.6 kwa kipindi cha miaka minne. Hawa ni watoto wa Kitanzania, wa Jimbo la Korogwe masikini, ambao uwezo wetu wa kulipa ada tungekuwa hatuna, na tungekuwa tunahangaika siku hadi siku, lakini sasa tunakaa tukifurahi kwa sababu watoto wetu wana uhakika wa kusoma bila kufukuzwa kwa ajili ya ada. Lakini katika elimu, pia tumejenga shule nyingi, madarasa mengi, na zaidi ya sh. bilioni 6.8 zimetumika”amesema CPA Njama.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi