March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwinyi kujengea mazingira rafiki wavuvi, wachuuzi, wajasiriamali

Na Is-haka Omar, Timesmajiraonline,Zanzibar

MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwajengea mazingira rafiki wananchi waliojiajiri katika fani za Uvuvi,Uchuuzi na Wajasiriamali ili waongeze kibato chao.

Amefafanua kuwa dhamira hiyo inatokana na maelekezo ya Sera za CCM zinazosisitiza umuhimu wa makundi yote ya wananchi kunufaika kupitia kazi wanazozifanya kwa lengo la kupata kipato halali cha kuendesha maisha yao ya kila siku.

Katika maelekezo yake Dk.Mwinyi amefafanua kuwa endapo kundi hilo watafanya usindikaji na upatikanaji wa samaki kwa wingi itasaidia wao kuongeza kipato chao kwa wingi sambamba na kukuza uchumi wa nchi.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Septemba 30, 2025, alipokutana na wavuvi, wachuuzi wa samaki na wajasiriamali wa Diko na Soko la Samaki la Malindi, wakati akiendelea na kampeni zake na kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi.

Amesema Serikali itaandaa utaratibu mzuri wa usimamizi wa masoko ili kumaliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wajasiriamali katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaongeza fedha za mikopo maradufu, kutoka Shilingi Bilioni 96 zilizotolewa awali, na kusisitiza kuwa wale ambao hawakupata katika awamu ya kwanza watapatiwa nafasi katika awamu inayofuata.

“Nimefurahi sana kukutana nanyi. Naomba kura zenu kwangu, kwa mama Samia Suluhu Hassan na wagombea wengine wa CCM. Niliyoyaahidi mwaka 2020 nimefanikiwa kuyatekeleza, na sasa naomba tena miaka mitano ijayo ili tuzidi kushirikiana katika kuleta neema zaidi,” alisema Dk. Mwinyi.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali yake imetoa mikopo isiyo na riba, maboti kwa wavuvi pamoja na vifaa vya kilimo cha mwani, hatua ambayo ni mwanzo wa safari ndefu ya kuwawezesha wavuvi na wakulima kuongeza kipato.

Kupitia ziara hiyo,Dk.Mwinyi ameahidi kuendeleza ujenzi wa madiko na masoko ya samaki ya kisasa pamoja na maeneo ya wajasiriamali Unguja na Pemba, sambamba na kuwapatia wavuvi boti na vitendea kazi vya kisasa vitakavyowawezesha kufanya uvuvi wa bahari kuu kwa ufanisi zaidi.

Pamoja na hayo Dkt. Mwinyi, ametoa wito kwa makundi hayo na wananchi kwa ujumla kumchagua tena ili aendelee kutekeleza ahadi zake na kuleta maendeleo zaidi kwa Zanzibar.

Katika ziara hiyo ya kampeni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,aliwambia wajasiriamali hao kuwa Mgombea huyo Dk.Mwinyi aliteuliwa na CCM kutokana na uwezo wake wa kuleta maendeleo endelevu kwa kila mwananchi.

Aliwasihi ifikapo Octoba 29,mwaka huu wamuunge mkono kwa kumpigia kura yeye pamoja na Wabunge,Wawakilishi na Madiwani wote wa CCM ili iendeleze miradi na mafanikio yanagusa maisha ya wananchi wote.

Akizungumza Mohamed Said Juma ambaye ni Mvuvi wa Diko hilo,alimpongeza Dk.Mwinyi kwa kazi kubwa ya kuleta mageuzi makubwa kwa kuwajengea mazingira rafiki ya kufanya biashara zao kwa uhakika bila kuwepo usumbufu wa kodi na kuhamishwa bila utaratibu.

“Naipongeza Serikali ya Zanzibar chini ya Dk.Mwinyi wamefanya kazi kubwa na yakupigiwa mfano kwani Diko letu la hivi sasa sio la miaka 10 iliyopita kwa sasa tunafanya kazi zetu katika mazingira salama”,,alisema Mohamed.

Naye Fatma Mussa Haji Mjasiriamali wa Diko na Soko la Samaki la Malindi,alipongeza juhudi za Serikali za kuwajengea soko hilo la kisasa lenye miundombinu rafiki ya kuhifadhi na kufanya kazi zao kwa uhakika.

……………………………………………………….

Dkt. Nchimbi aanika makubwa
yaliyofanywa na Rais Samia

Na Agnes Alcardo

MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika eneo la uwekezaji na diplomasia ya uchumi, hatua iliyosaidia kuvutia wawekezaji wengi na kuchochea ukuaji wa biashara nchini.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Kampala, Gongo la Mboto, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Nchimbi alisema takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Samia, idadi ya wawekezaji wakubwa walioingia nchini imeongezeka kutoka wastani wa 207 hadi kufikia 901.

Aidha, alisema leseni mpya za wafanyabiashara zilizotolewa zimepanda kutoka 137,508 miaka mitano iliyopita hadi kufikia 222,459 mwaka huu.

“Katika eneo la uwekezaji kazi kubwa imefanywa na Rais Samia na Serikali ya CCM. Tumeshuhudia ongezeko la wawekezaji wakubwa na utoaji wa leseni nyingi zaidi kwa wafanyabiashara wetu, hatua inayothibitisha kwamba Tanzania imekuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji Afrika,” alisema Nchimbi.

Aidha, alitaja sekta ya elimu kuwa ni eneo jingine ambalo Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwa nguvu kubwa.

Alisema Rais Samia amewezesha ajira mpya kwa walimu wa shule za msingi 38,394 na walimu wa sekondari 16,000, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu nchini.

“Rais wetu ametambua umuhimu wa elimu na ameipa kipaumbele cha pekee kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora,” alisema.

Aidha, Dkt. Nchimbi alisema lakini chama hicho kimepanga kwenye maeneo ya mijini kutoa mafunzo kwa vijana ya ujasiriamali na ufundi ili waweze kujiajiri.

Kabla ya kuzungumzia mitano ijayo, CCM itawafanyia nini Watanzania, alisitisha hotuba yake kutoa heshima kwa adhana ya kukaribisha waumini wa kiislamu kwa ajili ya swala ya adhuhuri.

Baada ya hapo alisema Serikali ya CCM imepanga kuendeleza utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara zaidi ya 20 kwa kiwango cha lami na changarawe katika Jimbo la Ukonga, na kukamilisha barabara ya Mwendokasi kutoka Nyerere, Pugu hadi Gongo la Mboto.

Pia, alisema miradi ya maji zaidi ya 10 itatekelezwa ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 79 hadi 90 kwa kila watu 100.

Vilevile, alisema serikali imepanga kujenga hospitali mpya ya yenye hadhi ya wilaya katika eneo la Pugu, vituo vipya vya afya vitatu na kupanua kituo cha afya cha Chanika.

Katika sekta ya elimu, alisema shule za msingi 250 na shule mpya za sekondari 304 zitajengwa ili kukabiliana na ongezeko la watoto. “Pamoja na hayo, vijana watapatiwa mafunzo ya ufundi na ujasiriamali mijini ili kuwawezesha kujiajiri.”

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ukonga kupitia CCM, Jerry Silaa alisema maendeleo yaliyopatikana katika jimbo hilo yanathibitisha dhamira ya Rais Samia kuwaletea wananchi mabadiliko makubwa.

Alitaja ujenzi wa barabara za ndani, madaraja, soko jipya na upanuzi wa huduma za afya kuwa ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha miaka minne na nusu.

“Jimbo la Ukonga limepata fedha zaidi ya sh. bilioni 233 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na mradi wa DMDP ambao unajenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 74,” alisema.

Silaa aliongeza kuwa kila kata kati ya 13 za Jimbo la Ukonga imepatiwa kituo cha afya kipya au ukarabati mkubwa, huku akisisitiza kuwa wananchi wa Ukonga wameamua kumpa tena kura Rais Samia na wagombea wa CCM kutokana na kazi iliyofanyika.

Mratibu wa Kampeni Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Mary Chatanda aliwataka wananchi wa Ilala na Ukonga kwa ujumla kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kumpigia kura Rais Samia, wagombea wa ubunge na udiwani wa CCM.

“Akina mama wa Ukonga na Kivule wanasema wamepatiwa heshima kubwa na chama chetu kumteua mwanamke kuwa mgombea urais. Wameahidi kurudisha heshima hiyo kwa kumpa kura za kishindo Rais Samia,” alisema Chatanda.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Kuu ya Taifa, Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Haji Issa Gavu aliwahimiza wananchi waendelee kuiamini CCM na wagombea wake kwa kuwa chama hicho kimeonesha uzoefu, nia na uwezo wa kuendelea kuiongoza nchi.

“Kwenye uongozi, msije mkajaribu mambo yasiyo na uhakika. Chama chetu kina uzoefu, kina dhamira na tayari kimeonyesha matokeo. Kwa hiyo tarehe 29 Oktoba, tumchague Rais Samia, wabunge na madiwani wa CCM ili tuendelee kusonga mbele,” alisema.

Mwisho””””””””””””””””””””””