March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazindua mafunzo ya ndani  watekelezaji mradi wa mawasiliano Vijijini

Na Irene Clemence,Timesmajiraonline,Dar

SERIKALI kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezindua rasmi mafunzo ya ndani ya nchi kwa watekelezaji wa Mradi wa Mawasiliano Vijijini (Tanzania Mobile Network for Rural Coverage Project – TMN4RCP), ikiwa ni hatua muhimu katika kufikisha huduma za mawasiliano hadi maeneo ya vijijini kote nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 29,2025 Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka wizara hiyo, Salome Kessy, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, awe mjini au kijijini, anapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano ya simu, mtandao wa intaneti, na usikivu wa redio kupitia TBC Taifa.

“Katika dunia ya sasa inayosukumwa na maendeleo ya kidijitali, hakuna taifa linaloweza kupiga hatua bila kuwa na mawasiliano ya uhakika. Mafunzo haya ni muhimu kwa kuwajengea uwezo wataalamu wetu kusimamia kwa weledi miradi ya TEHAMA hususan maeneo ya vijijini,” alisema Kessy.

Amesema Mafunzo hayo yanahusisha teknolojia za kisasa kama uboreshaji wa mitandao ya simu vijijini (2G na 4G), teknolojia ya LTE, mitandao ya msingi (Core Network), pamoja na mbinu za kukabiliana na changamoto za mawasiliano ya sauti, intaneti na malipo vijijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku, amesema  mradi wa TMN4RCP ulizinduliwa rasmi Desemba 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026, kwa lengo la kuhakikisha asilimia 100 ya maeneo ya kijiografia ya Tanzania yanapata huduma za mawasiliano na usikivu wa redio.

“Hadi sasa huduma za mawasiliano zinafikia asilimia 75 pekee ya maeneo ya nchi. Kupitia mradi huu, tunalenga kujenga jumla ya minara 636—ambapo 621 ni kwa ajili ya simu na 15 kwa ajili ya redio zitakazoendeshwa na TBC,” amesema  Munaku.

Ameongeza kuwa mafunzo ya ndani yanayofanyika sasa yanawahusisha wataalamu 140 kutoka TTCL na TBC, huku wengine 3,372 walishapatiwa mafunzo nchini China mapema mwaka huu, kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi, Kelvin Mwakaleke, amesema Serikali ilisaini mkataba wa utekelezaji na kampuni ya China Technical Import and Export Corporation (CNTIC) tarehe 23 Oktoba 2023 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 108.5, fedha ambazo ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya China.

“Utekelezaji wa mradi huu wa miezi 24 umefikia asilimia 56 kufikia Septemba 29, 2025. Kati ya minara 621 ya simu, upembuzi yakinifu wa minara 467 umekamilika, 261 imejengwa na 130 kati yake tayari inatoa huduma,” alifafanua Mwakaleke.

Aidha,amesema  ujenzi wa minara 15 ya redio unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 30 mwaka huu. Ufungaji wa miundombinu ya mawasiliano katika ofisi za TTCL Dar es Salaam na Dodoma umekamilika kwa asilimia 90, huku ugomboaji wa vifaa ukiwa umefikia asilimia 65.

Amesema Mafunzo hayo ya ndani, yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 7, 2025, yanalenga kuwajengea uwezo wataalamu katika maeneo ya Radio Access Network (BTS Systems), Transmission (Backhaul Systems, Civil Works), na mbinu za kiufundi za kuimarisha mawasiliano ya simu vijijini.