March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIC yaendelea kutoa elimu na huduma za Bima katika Kijiji cha Bima katika maonyesho ya Madini

Na Mwandishi wetu Geita

NIC inaendelea kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu na huduma za bima kwa wananchi kupitia Kijiji cha Bima kilichoko kwenye Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

Kijiji cha Bima ni mkusanyiko wa watoa huduma mbalimbali wa bima nchini, waliounganishwa chini ya uratibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa lengo la kutoa elimu, ushauri na huduma za bima kwa wananchi na wadau wa sekta ya madini na biashara.

Akizungumza katika Banda la NIC lililopo katika Kijiji cha Bima,Afisa Uhusiano wa NIC Ephrasia Mawala amesema NIC kama taasisi ya umma inayojikita katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima, inatoa huduma za bima ya maisha, bima ya mali, bima kwa wachimbaji pamoja na ushauri juu ya aina sahihi za bima kwa mazingira mbalimbali ya kibiashara na kijamii.

Amesema ushiriki wa NIC katika Kijiji cha Bima ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo ya kuendelea kufikisha elimu ya bima kwa wananchi kwa njia rahisi na ya moja kwa moja, kwa kushirikiana na mamlaka na taasisi nyingine. 

Maonesho haya ni fursa muhimu ya kuwasogezea wananchi elimu ya kifedha, hasa kupitia bima, ambayo ni nyenzo ya msingi ya kujikinga na athari za kiuchumi zitokanazo na majanga mbalimbali.

Amewakaribisha wananchi wote  kutembelea banda la TIRA – Kijiji cha Bima, ili kupata huduma na maelezo kutoka kwa NIC pamoja na watoa huduma wengine wa bima waliopewa kibali cha kutoa huduma chini ya usimamizi wa TIRA.