Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
SPIKA wa Bunge na Mgombea Ubunge Jimbo jipya la Uyole kupitia CCM,Dkt.Tulia Ackson, amesema changamoto ya maji katika Kata ya Itezi iko mbioni kumalizika kutokana na hatua ya kuchimba visima inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Akizungumza Oktoba 25, 2025, wakati wa kampeni zake Itezi,Dkt. Tulia alisema tayari kisima cha maji kimeanza kuchimbwa katika Mtaa wa Igombe na kazi inaendelea.
“Changamoto ya maji hapa Itezi naifahamu vizuri kwa sababu mimi pia ni mkazi wa Uyole. Tayari tumeanza kuchukua hatua za utekelezaji kwa kuchimba visima. Kuna mradi wa Savotusi unaotoka Mbeya Vijijini na mradi mwingine wa African Spring, wote watasaidia kuondoa kero ya maji. Niliwaahidi na sasa utekelezaji unaonekana, na bado tunaendelea kuhakikisha upatikanaji wa maji unatosheleza,” amesema.

Ameongeza kuwa wadau mbalimbali wamejitokeza kusaidia, na kisima kingine kinatarajiwa kuchimbwa Tambureli ili watoto waachane na kubeba ndoo za maji na wananchi wapate huduma bora kutokana na visima vya kina.
Aidha, Dkt. Tulia amesema nia ya CCM ni kuhakikisha maji ya uhakika yanapatikana, huku akitaja mradi mkubwa wa Kiwira ambao tayari umeanza utekelezaji na kuahidi kuwa utatatua tatizo hilo kwa wananchi wengi zaidi.
Kuhusu miundombinu, Dkt. Tulia amebaisha kuwa barabara za mitaa katika Uyole zitaboreshwa ili wananchi wafanye shughuli zao bila changamoto. Alisema fedha za fidia kiasi cha Sh bilioni 27 tayari zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya mchepuko, yenye lengo la kupunguza msongamano wa malori na ajali za mara kwa mara.
Kwa upande wake, Diwani Mteule wa Kata ya Itezi, James Kapolesya, ameomba mtaa wa Mwasote pia ujengewe kisima cha maji ili kuondokana na adha inayowakabili wakazi wa eneo hilo.
“Mheshimiwa Mbunge, kwanza nakushukuru kwa jitihada za barabara za nje nne, ni kazi kubwa. Hata hivyo, bado kuna mitaa yenye changamoto kubwa, hususan maeneo yenye majengo mapya. Pia tunaomba kisima kipatikane Mwasote, kama walivyopata wenzetu wa Gombe,” amesema Kapolesya.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako