Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimejipanga kuendelea kushughulikia changamoto za wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, umeme na miundombinu, sambamba na kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 24, 2025 na Mgombea Ubunge Jimbo jipya la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, wakati akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika mtaa wa Ituha, kata ya Ilomba.
Amesema wananchi wanapaswa kuendelea kuwa na imani na CCM kwa kuwa ni chama kilichojipanga kuhakikisha wananchi wa Uyole wanapata huduma muhimu bila changamoto.
“Ndugu zangu wa Ituha, naombeni kura za kishindo kwa Rais Samia na kwa nafasi yangu ya ubunge. Tukiipatia CCM ridhaa ya kuongoza katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, tutajitahidi kumaliza changamoto zinazowakabili, ikiwemo huduma za maji na miundombinu ya kisasa,” amesema Dkt. Tulia.
Akitolea mfano sekta ya elimu, alisema CCM imefanikisha ujenzi wa Shule ya Msingi Tonya, madarasa mapya, na maboresho ya mazingira ya kujifunzia, ikiwemo kumaliza tatizo la uhaba wa madawati. Aliongeza kuwa Shule ya Sekondari Ilomba imeboreshwa na kujengwa Shule ya Sekondari Ikulu, huku wanafunzi kutoka familia zenye mazingira magumu wakipatiwa sare na daftari.
Kuhusu changamoto ya maji, Dkt. Tulia amesema utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Mto Simba umeshaanza, huku mradi mkubwa zaidi wa Mto Kiwira ukitarajiwa kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wa Ilomba na maeneo jirani.
Aidha, amehaidi kuhakikisha barabara zote za kata hiyo zinajengwa kwa kiwango cha lami, zikiwemo za kuunganisha Ilomba na Uyole kupitia barabara ya Roma–Ituha–Nsongwi Juu, ili kupunguza usumbufu wa wananchi.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Ilomba, Nour Mwakisu, aliwataka wananchi kumthamini Dkt. Tulia, akimtaja kuwa “bidhaa adimu” kutokana na jitihada zake za kupeleka maendeleo katika maeneo mbalimbali.
“Tumeshuhudia fedha nyingi zikielekezwa katika miradi ya elimu, barabara na maji. Hapa Ilomba tumepata shule mpya, maabara, barabara bora, na hata tuliposikia ahadi zako za kupunguza vumbi, tumeona utekelezaji wake,”alisema Mwakisu.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako