March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THBUB yatoa wito kwa vyombo vya habari

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB)imetoa wito kwa vyombo vya habari kujikita katika kuimarisha amani,utulivu na demokrasia nchini kwa kutotumia vibaya kalamu zao.

Pia imewataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.

Wito huo umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa THBUB, Patience Ntiwa wakati akifungua mafunzo kwa Waandishi wa habari wa Mkoa wa Dar es Salaam kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.

Amesema waandishi wa habari wanawajibu wa kuepuka kutumia lugha ya matusi,kafsha,kejeli,udhalilishaji au vitisho katika kuripoti matukio ya uchaguzi.

Ntiwa amesema mbali na hayo waandishi wa habari wanapaswa kuepuka rushwa,takrima au zawadi zenye lengo la kushawishi maudhui yenye kuegemea upande wa chama au mgombea fulani.

”Mafunzo haya yatasaidia kuweka misingi ya kitaaluma na maadili kwa vyombo vya habari,waandsihi wa habari na wadau wote wa sekta ya habari kwa madhumuni ya kuhakikisha haki ,usawa na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma ili kukuza demokrasia nchini,”amesema na kuongeza

”Mafunzo haya yatasaidia kulinda amani na utulivu kwa taifa na kuepusha kuchapisha maudhui yenye viashiria vya uchochozi,upoteshaji,kuegemea upande mmoja au yasiyo na uthibitisho,”amesema.

Alisema katika kipindi cha uchaguzi,waandishi wa habari wanawajibu wa kuripoti habari na matukio yote ya uchaguzi kwa usahihi bila upendeleo kwa chama,mgombea au msimamo wowote wa kisias na kuweka uwiano sawia wa taarifa kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi

.

Ntiwa alisema katika muktadha wa uchaguzi ulio huru na wa haki na wenye kuzingatia misingi ya demokrasia,vyombo vya habari vinanafasi ya kipekee katika kuhakikisha kunakwepa upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma.

Alisisitiza kuwa vyombo vya habari ni daraja kati ya wagombea,vyombo vya siasa,Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wananchi ambapo vyombo hivyo vinachangia kwa kiasi kikubwa kujenga uelewa wa wapiga kura kuhusu sera na ajenda za kisiasa.

Kwa upande wake mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo,Kilua Mtae alisema haki za binadamu katika uchaguzi zimezingatia katika sheria mbalimbali za kimataifa,Kikanda na Kitaifa.

Alisema miongoni mwa haki hizo ni pamoja na kushiriki katika shughuli za umma,haki ya kutoa maoni,kutoa taarifa na kutobaguliwa.”Katika mikataba ya kimataifa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imeridhia mikataba ya kimataifa ya kulinda haki za binadamu ikiwemo ibara ya 21 ibara ndogo ya kwanza inayosema haki ya kushiriki katika shughuli za umma,”alisema.

Naye Mtoa mada wa Pili kutoka katika ofisi ya Tume hiyo, Philomeno Thomas alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha waandishi wa habari namna ya kutoa taarifa kipindi cha uchaguzi ikiwemo kufanya kazi kwa kuzingatia ukweli,kuripoti taarifa zilizosahihi na zilizodhibitishwa,uhuru na mgongano wa kimaslahi na kuhakikisha kuepuka kuandika kwa ushawishi na maslahi binasfi au kwa taasisi.