March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu atembelea Banda la NSSF, aelezwa mafanikio ya kidigitali katika kuhudumia sekta binafsi

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online ,Geita

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, na kupewa maelezo kuhusu maboresho makubwa yanayofanywa na mfuko huo katika kuhudumia wananchi, hususan walioko kwenye sekta binafsi na waliojiajiri.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo Sept 22,2024 Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bw. Masha Mshomba, amesema kuwa mafanikio ambayo NSSF imeyapata ni matokeo ya maelekezo ya viongozi wa serikali, akiwemo Waziri Mkuu mwenyewe.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili ni banda lako. Mafanikio ambayo tunajivunia leo hii ni matokeo ya uongozi thabiti wa serikali. Mmetuelekeza tutoe huduma bora, kwa wakati, na kwa njia rahisi. Sisi kama NSSF tumechukua maelekezo hayo na kuyatekeleza kikamilifu,” amesema Bi. Lulu mbele ya Waziri Mkuu.

Ameeleza kuwa NSSF kwa sasa imejikita katika kutoa huduma kwa njia za kidijitali, ambapo mwananchi anaweza kupata taarifa zake zote muhimu kupitia simu ya mkononi kwa urahisi. “Leo hii, mwananchi anakuja na simu yake tu, anascan QR code na ndani ya muda mfupi anapata taarifa zake zote iwe ni kuhusu michango, ajira, au matibabu,” alifafanua.

“Katika kuendana na mageuzi ya teknolojia, NSSF inalenga kuwafikia makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo wachimbaji wadogo, mama lishe, na wajasiriamali wengine walio katika sekta isiyo rasmi. “Mnatuelekeza tufanye huduma iwe ya kidigitali, iweze kumfikia kila Mtanzania, na sisi tuko hapa kutekeleza hilo,” amesisitiza Bi. Lulu.

Bi. Lulu ameongeza kuwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Sita, thamani ya Mfuko wa NSSF imeongezeka kutoka Sh trilioni 4.8 hadi Sh trilioni 9.8, ikiwa ni ishara ya usimamizi thabiti na ufanisi mkubwa wa mifumo ya hifadhi ya jamii nchini.

“Tuko hapa si kwa ajili ya kuonesha tu tunachofanya, bali kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi. Tunataka kila mmoja ajue kuwa mfuko huu ni wake na sasa unamfikia moja kwa moja kupitia teknolojia rahisi,” amesema.