Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Geita
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Mboni Mhita, ametembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Septemba 22,2025.
Katika ziara hiyo, Bi. Mhita aliipongeza DIB kwa kazi kubwa inayofanya katika kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha nchini, akibainisha kuwa mchango wa taasisi hiyo ni wa msingi kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akiwa kwenye banda hilo, Bi. Mhita alipata maelezo ya kina kuhusu majukumu ya Bodi ya Bima ya Amana, ikiwa ni pamoja na kusimamia mfuko wa bima ya amana kwa ajili ya kuhakikisha ulinzi wa wateja wa benki na taasisi za fedha.
Majukumu mengine ya DIB ni pamoja na kulipa fidia kwa wateja iwapo benki au taasisi ya fedha itafungwa na kushindwa kulipa amana zao, sambamba na kusimamia mchakato wa ufilisi wa taasisi hizo kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania.
Aidha, alielezwa kuwa Bodi hiyo hufanya kazi kwa karibu na mamlaka za fedha nchini kuhakikisha ulinzi wa amana za wananchi na kuimarisha imani kwa mfumo wa fedha rasmi.
Bi. Mhita pia aliambiwa kuwa kuanzia Julai 2025, DIB imeongezewa jukumu jipya la kuwa “loss minimiser”, yaani kupunguza hasara katika benki au taasisi ya fedha zinazopitia changamoto za kifedha ili zisifikie hatua ya kufungwa.
Mkuu huyo wa Mkoa alihitimisha kwa kupongeza juhudi za DIB katika kulinda maslahi ya wananchi na kusisitiza kuwa elimu kuhusu bima ya amana iendelee kutolewa ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani