



Na Joyce Kasiki,Timesmajira online ,Dodoma
KATIBU Mkuu ,Wizara ya Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo amefanya ziara katika jengo la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Tume hiyo inayojengwa jijini Dodoma huku akiiagiza kuhakikisha inajenga na kuboresha kumbi zitakazotumika kuwaatamia na kuwaendeleza wabunifu chipukizi nchini, ili waweze kukuza bunifu zao na kuzigeuza kuwa bidhaa za kibiashara zitakazotatua changamoto katika jamii nchini.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kupata taarifa ya ujenzi chini ya mradi HIT, Prof. Nombo amesema kuwa ujenzi wa kumbi hizo ni sehemu ya mkakati wa serikali kuhakikisha vijana wabunifu wanapata mazingira bora ya kuendeleza maarifa yao, hatimaye kuzibadilisha kuwa bidhaa au huduma zitakazowapeleka kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Nawapongeza COSTECH kwa hatua mliyofikia ya ujenzi. Hii inaonyesha mnavyotekeleza kwa vitendo agizo la serikali la kuzitaka taasisi zake zihamie Dodoma,” amesema Prof. Nombo.
Katika ziara hiyo, Prof. Nombo pia alimhimiza mkandarasi wa kampuni ya Till anayesimamia ujenzi huo, kuwajumuisha vijana wanaosomea fani mbalimbali katika vyuo vya ufundi kama VETA, ili wapate mafunzo ya vitendo kwa lengo la kuwaandaa ipasavyo kwa soko la ajira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema ujenzi wa ofisi hiyo umeanza Machi mwaka huu na inarajiwa kukamilika Machi 2026.
Aidha Dkt.Nungu amesema katikanofisi hiyo kutakuwa na kumbi za kulelea bunifu mbalimbali kwa kipindi cha hadi miaka miwili kabla ya wabunifu hao kuhitimu na kuanzisha kampuni zao au kujiajiri.
Dkt. Nungu aliongeza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya sayansi na teknolojia kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi nchini, huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina