Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
BODI ya shirika lisilo la kiserikali la Child Support Tanzania(CST), linalojihusisha na malezi ya watoto wenye ulemavu, imesema imeweka mikakati ya kuifikia jamii kwa kutoa elimu jumuishi na shirikishi, ikiwa na lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu bora bila kujali hali yake.
Hayo yamesemwa Septemba 9, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Radio Dream FM, Mhandisi. Jameson Kasati wakati wa mjadala wa elimu jumuishi na usawa wa kijinsia uliohusisha wazazi, walezi, walimu, watoto wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu, maafisa elimu pamoja na Dawati la Jinsia na Watoto.

Mha.Kasati amesema bodi hiyo imepanga mikakati mbalimbali ya kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika kupata elimu bora.
“Jamii zetu bado zina kasumba mbalimbali kuna imani kwamba elimu fulani ni kwa watoto wa kike au wa kiume pekee na hata teknolojia fulani ni kwa watu wa aina fulani. Tunachofanya sasa ni kutoa elimu kupitia njia mbalimbali, tukishirikiana na mamlaka za serikali ili kuboresha miundombinu na kufikia watoto wengi zaidi,” amesema.
Aidha, amewataka wazazi kubadilisha mitazamo hasi dhidi ya watoto wenye ulemavu, akisisitiza kuwa ulemavu si adhabu, bali watoto hao ni baraka za Mwenyezi Mungu.
Mha.Kasati ameongeza kuwa changamoto kubwa inayokwamisha elimu jumuishi ni miundombinu ya zamani ambayo haikuzingatia ushirikishwaji wa watoto na watu wenye ulemavu. Alitoa rai kwa serikali kuhakikisha miundombinu mipya inajengwa kwa kuzingatia ujumuishi, huku ya zamani ikiboreshewa ili iwe rafiki kwa wote.
Kwa upande wake, Bilievi Mwaisela, mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Iyunga na mwenye ulemavu, amesema jamii bado inawanyanyapaa watoto wenye ulemavu, huku baadhi ya familia zikihusisha hali hiyo na imani za kishirikina.

“Nawaambia watoto wenzangu wenye ulemavu wasikubali kukatishwa tamaa ya kusoma. Nimefika hapa kwa ujasiri wangu na kuthubutu licha ya hali niliyonayo. Wapo wazazi wanaodhani elimu haina umuhimu kwetu, lakini ukweli ni kwamba tuna uwezo sawa,” amesema Bilievi.
Naye SGT Consolata Mng’ong’o,kutoka Dawati la Jinsia na Watoto katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, alisema jamii inapaswa kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha watoto wenye ulemavu hawafichwi ndani.
“Watoto wenye ulemavu si wagonjwa, bali ni hali waliyozaliwa nayo. Tunapita kutoa elimu kwa jamii, lakini bado wazazi wengi hukumbana na changamoto ya kuchekwa. Aidha, shule zenye wataalamu wa kufundisha watoto wenye mahitaji maalum ziko mbali, hivyo tunaiomba serikali kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wenye ujuzi huo,” amesema.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi