Na Bakari Lulela
MKURUGENZI wa Ofisi ya Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga, amesema mantiki ya kutenganisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya DDP ni kuleta mabadiliko ya kiufanisi katika utendaji wa kazi zilizokuwa zikifanywa na taasisi hizo.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mashtaka nchini,Mganga, amesema mabadiliko hayo yametokana na majadiliano ya Tume ya Msekwa iliyoundwa mnamo mwaka 1976 na ya Jaji Bomani ya mwaka 1996.
Amesema Tume hizo ziliamuru kutenganishwa kwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa lengo la kufanyakazi kwa ufanisi.
Mganga amesema mchakato huo ulifanyika kwa kushirikisha Tume hizo, ambapo kulibainika kuwa haitawezekana ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iweze kusimamia shughuli za mashtaka na pia kuishauri Serikali.
Aidha,kupitia maoni ya Tume hizo, mwaka 2005 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliweka wazi majukumu ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hata hivyo ofisi hizo zilifanyakazi kwa kushirikiana.
Mkurugenzi huyo wa mashtaka alisema kuwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ndio yenye mamlaka kusimamia majukumu yote ya mashtaka, isipokuwa kutakuwa na watu watakao kuwa wakimsaidia katika uendeshaji wa shughuli hizo.
Mganga ameeleza kuwa mwaka 2008 ofisi za mashtaka zilisambazwa katika baadhi ya mikoa ikiwemo Arusha, Moshi, Mtwara na Dar es Salaam ili huduma ziwe karibu na wananchi.
Kwa mujibu wa Mganga Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, Rais alianzisha rasmi Ofisi ya Mashtaka ili kuhakikisha kesi zote za jinai zinaendeshwa kwa wakati.
Akizungumzia kuhusiana na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali Awamu ya Tano, alisema mengi yamefanikiwa ikiwa ni pamoja na kusikiliza na kutoa hukumu za kesi za mafisadi, wauzaji dawa za kulevya na watoroshaji wa madini,wauzaji pembe za ndovu na wengine wengi.
Ameongeza kwamba wamefanikiwa kutaifisha mali zinazotokana na kesi za uhalifu, ambapo hadi sasa wametaifisha magari 143. Kati ya magari hayo, 132 yamekabidhiwa kwa Serikali.
Mali nyingine ni pikipiki 163, nyumba 23, mashamba matano ambapo moja lilikuwa na hekari tano lililokuwa pembezoni mwa ziwa Victoria.
“Kutaifishaifisha kwa mali hizi kumesaidia kupunguza kesi nyingi za uhalifu nchini, kwani jamii sasa inatumbua kuwa unapokutwa na mali iwe ni fedha ambazo zimetokana na uhalifu Serikali inazitaifisha mali zote za mtuhumiwa,” amesema.
Mganga amesema katika kipindi cha nyuma baadhi ya maaskofu walikuwa wakijipatia mali kwa kutumia majina viongozi wakubwa ambao wengi wao wamefungwa.
Akizungumzia kuhusiana na wizi uliokuwa ukitumika kwa kutumia ujumbe mfupi maarufu kama Tuma pesa kwa namba hii, Mganga alisema wengi wao wamekamatwa na kifungwa.
“Tabia hiyo naamini bado haijaisha…hata mimi juzi nimepokea ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi wa kutaka kuniibia, hivyo tunaendelea na uchunguzi wa kubaini wengine waliobaki na tunawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa,” amesema.
Hata hivyo aliwaomba wananchi kuzingatia sheria za mtandaoni kwa kuacha kukubali kuandika ujumbe ambao unaweza kusababisha amani kutoweka nchini.
“Tusikubali kurubuniwa kwa kutaka kwenda kufanya maandamano ambayo wahusika wakuu wanakuwa mbali na hata nje ya nchi, kwani mwananchi atakayekubali kufanya hivyo atakuwa anavunja sheria, hivyo atashkiwa na kusababisha wazazi, ndugu na hata watoto kupata tabu,” amesema.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ