Na Isaack Zenda,Tumaini University,Timesmajira
WAFANYABIASHARA wa Soko la Kisutu, jijini Dar es Salaam, wamelalamikia changamoto kadhaa zinazokwamisha maendeleo ya biashara zao, ikiwemo miundombinu chakavu, uhaba wa wateja na biashara holela za barabarani.
Maulid Ramadhan, Mfanyabiashara na Mkazi wa Karakata, amesema moja ya matatizo makubwa ni hali ya vyoo, ambavyo vimeharibika na kuvuja maji, hali inayohatarisha afya za wafanyabiashara na wateja.
“Vyoo vya chini vina maji yanayovuja kutoka juu. Hili ni tatizo kubwa linalohitaji kufanyiwa ukarabati wa haraka. Vilevile, vifaa kama milango, kufuli na komeo huharibika mara kwa mara kutokana na wingi wa watumiaji, hivyo vinahitaji matengenezo ya mara kwa mara,” amesema.
Akizungumzia changamoto za kibiashara, Ramadhan amesema tatizo kubwa ni uhaba wa wateja kutokana na bidhaa zinazouzwa sokoni kupatikana pia mitaani kwa urahisi.
“Ni kweli sokoni bidhaa zinapatikana kwa wingi, lakini wateja wachache kwa sababu wanazipata mitaani pia. Hii inasababisha biashara kudorora wakati soko hili lilijengwa kwa matarajio ya kukuza biashara,” ameeleza.
Ameongeza kuwa kuhamishwa kwa makao makuu ya serikali kwenda Dodoma kumechangia kudhoofisha biashara, kwani watumishi wa umma waliokuwa wateja wakuu wa soko walihamia huko pamoja na ofisi zao.
Ramadhan pia alilalamikia biashara holela za barabarani akisema hatua hiyo inapunguza wateja wa soko hilo la ghorofa.
“Kama serikali imewekeza fedha nyingi kujenga masoko ya kisasa, inapaswa kuhakikisha yanafanya kazi kama ilivyokusudiwa na kuondoa biashara za barabarani zinazodhoofisha mapato ya soko,” amesisitiza.
Hata hivyo, ameeleza kuwa hali ya usalama ndani ya soko ni ya kuridhisha, akiwapongeza walinzi kwa uadilifu wao pamoja na uongozi wa soko kwa kusimamia biashara ipasavyo.
Wafanyabiashara hao wametoa rai kwa serikali kuchukua hatua za haraka kurekebisha miundombinu, kuhakikisha usafi na kuimarisha ufuatiliaji wa biashara, ili kulinusuru Soko la Kisutu lisizidi kupoteza mvuto wake.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi