March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utekelezaji umeme wa uhakika Kagera  waanza

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko,ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako, Ngara hadi Kyaka wilayani Misenyi na kituo cha kupoza
umeme cha Benako cha msongo wa kilovoti. 220/33.

Dkt.Biteko ameshuhudia utiaji saini huo leo,Agosti 25,2025 katika hafla iliyofanyika jijini hapa ambapo amesema kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ni moja ya maelekezo ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa na kiu ya kutekeleza ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Kagera  ya kupata umeme wa uhakika muda wote ili kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

” Kupitia mradi huu, Mkoa wa Kagera kwa mara ya kwanza na wenyewe unaingia kwenye gridi ya Taifa hasa na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme hususan katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Misenyi, Karagwe, Kyerwa  na maeneo mengine ya jirani, nawahakikishia watu wa Kagera kuwa Serikali imeshaamua mradi  huu ufanyike kwa wakati kwa  miezi 24 tu” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amesema, Kagera ambayo mahitaji yake ya umeme hayazidi megawati 47 baada ya muda itakuwa na uhakika mkubwa wa upatikanaji umeme kwani kutakuwa na njia mbalimbali za kufikisha  umeme mkoani humo ikiwemo Benako- Karagwe hadi Kayaka,  Nyakanazi- Biharamulo hadi Muleba na kuna mradi mwingine mkubwa  unaotarajiwa kujengwa kutoka Ibadakuli hadi Mbarara Uganda wa kV 400. Vilevile kuna mradi wa uzalishaji umeme wa Kakono wa megawati 87 ambao upo katika hatua za mwisho za kutafuta Mkandarasi.

Aidha Dkt.Biteko amewashukuru wafadhili wa mradi  ambao wametoa Dola za Kimarekani takriban milioni 105.6 huku akiagiza kuwa zitumike kwa usahihi ili kuwapa sababu wafadhili wengine kuendelea kusaidia miradi mbalimbali.

Pamoja na hayo Dkt.Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wananchi 1,014 wanaopisha mradi wanalipwa fidia yao  mapema iwezekanavyo yaani kuanzia mwezi septemba mwaka huu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange akizungumz katika hafla hiyo amesema kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa mkoani Kagera kwani wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba kwa muda mrefu sasa zimekuwa  zikiitumia umeme kutoka nchini Uganda takribani megawati 40 kupitia kituo cha kupoza umeme cha Kyaka ambacho kinapokea umeme kutoka Masaka, Uganda kupitia njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 132 kufuatia mkataba wa makubaliano baina ya Tanzania na Uganda.

Ametaja gharama za mradi huo kuwa ni shilingi bilioni 262.5 na utatekelezwa kwa muda wa miezi 24.

“Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Serikali  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo Mfuko wa Maendeleo wa Shirika la Wauzaji Mafuta Duniani (OPEC)  utachangia dola za Marekani milioni 60, Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi utachangia dola za Marekani milioni 30, Mfuko wa Maendeleo wa Saudia utachangia dola za Marekani milioni 13 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachangia dola za Marekani milioni 2.6 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi,”amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, amesema tukio hilo ni la kihistoria kwa kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo kunamaanisha kuwa mikoa yote iliyokuwa nje ya gridi ya taifa sasa inakuwa na mpango wa kuunganishwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajati Fatma Mwasa, ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa miradi hiyo kutekelezwa kwa manufaa ya Wanakagera.

Amesema kuwa Mkoa unatumia megawati 46, na kwamba kupitia miradi hiyo, mkoa utaunganishwa na gridi ya taifa, ambapo awali ni wilaya tatu pekee ndizo zilizokuwa kwenye gridi hiyo.

“Tunakwenda kuwa na umeme wa uhakika na viwanda vitafanya kazi kwa uhakika kwa kile tunachohitaji. Wanakagera tumeipokea miradi hiyo kwa mikono yote, kwani mkoa unakwenda kuongeza maendeleo zaidi,”amesema Hajati Mwasa.