Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt.Doto Biteko amesema watanzania hawana sababu ya kuogopa kutumia umeme kupikia kwani nishati hiyo ipo ya kutosha,salama na vipo vifaa vinavyotumia umeme kidogo kupikia chakula kikaiva kama inavyotakiwa.
Dkt.Biteko amesema hayo jijini hapa leo,Agosti 14,2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa programu ya utoaji majiko ya umeme kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) ambapo amesema kwa sasa watanzania wanaotumia umeme kupikia ni asilimia 4.2 tu ikiwa ni asilimia ndogo ukilinganisha na idadi hali ya watanzania wanaotumia umeme kwa sasa.

“Ni ukweli usiopingika kwamba kwa historia na mazoea tuliyonayo watu wanaamini kutumia umeme kupikia ni ghali sana na hivyo huikwepa nishati hiyo kwasababu ya hofu,”amesema.
Amefafanua kuwa tafiti zinaonesha majiko janja ya umeme yanaweza kutumia chini ya uniti moja ambayo ni sawa na sh.352 kuandaa mlo mmoja,ambapo ukitumia mkaa unaweza kutumia sh.2000 hadi 3000.
“Ukitumia umeme kupika chakula cha mlo mmoja unakuwa umetumia chini ya uniti moja ambayo ni sawa na sh.352 ikiwa ni tofauti endapo utatumia mkaa unaouzwa kati ya 2000 hadi 3000,kwa tafsiri hiyo kutumia umeme kupikia kiwango cha umeme kinakaribia sawa matumizi ya balbu za umeme za nyumbani.
“Ukitumia umeme kupika maana yake ni sawa na mtu anayetumia balbu kwenye matumizi ya nyumbani,tunataka kusukuma ajenda ya nishati safi lazima tuwe mfano,Majiko janja ya umeme yanaweza kupika chini ya uniti moja,matumizi ya umeme kwa kupika ni nafuu kuliko nishati nyingine,amesema.


Pamoja na hayo aliwataka Wafanyakazi wa shirika hilo kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia watanzania pamoja na kwenye utekelezaji wa ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Msimamie shirika hili kwa wivu kuhudumia watu ili kuondoa umasikini mkawe mabalozi wazuri wa matumizi ya nishati ya umeme katika kupika,Kila mfanyakazi anapaswa kuwa na aibu kuwa na kuni au mkaa nyumbani kwake kwajili ya kupikia aone fahari kutumia umeme ili mnapowambia watu wengine muwe mfano kuishi mnayoyazungumza,”amesema
Awali Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO,Balozi Zuhura Bundala ametaja lengo la Shirika hilo kuchangia juhudi za kitaifa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia ajenda ya Watanzania asilimia 80 watumie nishati safi ya kupikia ikifika mwaka 2034.
Hivyo amesema shirika hilo linataka kubadilisha fikra kwa jamii kwamba umeme ni matumizi yaliyozoeleka bali hata kupikia kwani kuna vifaa vya kupikia vinavyotumia umeme kidogo.
“Ndiyo maana tumekuja na programu ya ugawaji majiko kwa wafanyakazi wa shirika hili itakayosaidia kuanza kubadili fikra ya jamii kwa kuona wanachofanya TANESCO,
“Kupitia Mradi huu wananchi wataona TANESCO si shirika tu la umeme bali ni mshiriki hai wa kulinda mazingira kuboresha afya na kuhamasisha maendeleo endelevu,
“Kwani programu hii itahamasisha wananchi kutanua wigo kwa wananchi kutumia umeme majumbani na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa hivyo kupunguza uharibifu wa misitu yetu,”amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mku TANESCO Lazaro Twange amesema katika kutekeleza ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia TANESCO wamezindua majiko ya kisasa ambayo yanatumia umeme mdogo na kuivisha haraka ambayo watapewa wafanyakazi wa shirika hilo ili kuwa mabalozi wazuri wa nishati hiyo.
Amesema kuwa TANESCO wameanza kwa kugawa majiko ya umeme kwa wafanyakazi wa shirika hilo kwa bei ya ruzuku ambapo jumla ya majiko 10,0000 yatatolewa kwa wafanyakazi wa shirika hilo,huku mkakati wa shirika ni kuhakikisha kila mwananchi anatumia majiko ya umeme yenye gharama nafuu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Shirika hilo na menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na wafanyakazi.



More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro