March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia Aongoza Mapinduzi ya Umwagiliaji Kukabili Mabadiliko ya Tabianchi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji kwa kufanya uwekezaji mkubwa unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uzalishaji wa chakula, na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Kitaifa na Kimataifa (Nane Nane) katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Rais Dkt. Samia alisema serikali imewekeza katika ujenzi wa mabwawa, ukarabati wa skimu za umwagiliaji, na uchimbaji wa visima kwenye maeneo yenye changamoto ya ukame, hatua inayolenga kuongeza tija na kupunguza utegemezi wa mvua.

“Nataka kuona Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ikiendelea kufanya kazi kwa kasi, kuhakikisha huduma za umwagiliaji zinawafikia wakulima wote   wadogo, wa kati na wakubwa   ili kuongeza uzalishaji na uzalishaji wa mazao yenye tija,” alisema Rais Dkt. Samia.

Maeneo Makuu Yaliyotekelezwa

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, zaidi ya hekta 700,000 zimeendelezwa kwa miundombinu ya umwagiliaji na tayari zinatumika kwa kilimo. Aidha, hadi Juni 2025 skimu mpya 3 za umwagiliaji zimekamilika, skimu 7 zimekarabatiwa, mitambo 3 ya kuchimba mabwawa imenunuliwa, pamoja na mitambo 30 ya kuchimbia visima imepelekwa mikoani.

Serikali pia inaendelea kutekeleza miradi 780 ya umwagiliaji yenye jumla ya hekta 543,366, ikijumuisha ujenzi wa skimu mpya 63, ukarabati wa skimu 48, ujenzi wa mabwawa 114, ujenzi wa miundombinu katika mabonde 22 ya kimkakati, na mashamba makubwa 6 ya pamoja. Kukamilika kwa miradi hii kutaongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 727,000 hadi milioni 1.2.

Dhamira ya Serikali

Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha sekta ya kilimo inasimama imara ifikapo mwaka 2030, ikitumia teknolojia bora na miundombinu ya kisasa ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

“Mnyororo mzima wa kilimo kuanzia uzalishaji wa mbegu, uhifadhi wa mazao, umwagiliaji, hadi udhibiti wa ubora lazima ufanye kazi kwa ufanisi. Tumeongeza hamasa ili taasisi zote husika zishirikiane,” aliongeza.

Rais pia alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, kuhakikisha teknolojia zilizopo zinawanufaisha wakulima moja kwa moja.

Mitambo na Teknolojia Mpya

Katika maonesho hayo, Rais alishuhudia matumizi ya teknolojia mbalimbali za umwagiliaji, ikiwemo mifereji, mipira ya kunyunyizia maji, matone, na mitambo ya kuchimba visima. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema teknolojia hizo tayari zinatumika kwenye mashamba ya mbegu ya serikali yenye zaidi ya hekta 13,000, na kwamba Centre Pivot  mtambo mkubwa wa umwagiliaji umeanza kufanya kazi katika baadhi ya maeneo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Bw. Mndolwa, alisema Tume imepata fedha za kununua pampu 2,000 ambazo zitasambazwa kwenye maeneo yenye rasilimali za maji tayari, na inaendelea na mazungumzo na kampuni za PAG na Pro Agro kujenga viwanda vya kutengeneza mitambo ya umwagiliaji nchini. Hatua hiyo inalenga kuongeza ajira, kuongeza thamani ya fedha za ndani, na kurahisisha upatikanaji wa vifaa nchini.