Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma
MWENYEKITI wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya KKKT Arusha Road SACCOS, Ibrahim Sumbe, amesema kuwa Jukwaa hilo limekuwa chombo imara cha kuwainua kiuchumi wanachama wake na kuleta mshikamano katika kutatua changamoto za vyama vya ushirika mkoani humo.
Akizungumza katika kilele cha Maonyesho ya Nanenane mkoani Dodoma, Sumbe amebainisha kuwa jukwaa hilo lilianzishwa miaka minne iliyopita kwa lengo la kuunganisha vyama vya kifedha kama SACCOS na vyama vya mazao kama AMCOS ili kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kujenga nguvu ya pamoja katika sekta ya ushirika.
“Kupitia Jukwaa hili, kila chama hujifunza kutoka kwa mwenzake, changamoto zinazowakumba zinajadiliwa kwa pamoja na kutafutiwa suluhisho. Pia tunashirikiana katika shughuli za kijamii ili kuonyesha kuwa ushirika sio tu biashara bali pia ni huduma kwa jamii,” alisema Sumbe.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Jukwaa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kusaidia makundi yenye uhitaji, ambapo hadi sasa wamefanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo,kutoa misaada kwa vituo vya watoto yatima, watoto wenye ulemavu na wazee katika wilaya ya Kondoa na maeneo mengine ya mkoa wa Dodoma
Vile vile kuchangia zaidi ya shilingi milioni 14 kwa Hospitali ya Mlowa, ikiwa ni pamoja na vifaa tiba, vitanda na mashuka,kushiriki katika maonyesho na makongamano ya kitaifa na kimataifa kuonyesha bidhaa na huduma za wanachama wa ushirika
“Hii ni njia ya kuhakikisha kuwa ushirika una mchango wa moja kwa moja kwa jamii. Tunajivunia kutoa huduma kwa watu wenye uhitaji kama sehemu ya maadili ya ushirika,” aliongeza Sumbe.
Kwa mwaka huu, Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Dodoma limepokea tuzo ya Jukwaa Bora Kitaifa, ikiwa ni ishara ya kuthaminiwa kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha ushirika nchini. Aidha, Jukwaa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kushiriki makongamano ya kimataifa, ikiwemo yale yaliyofanyika Uganda, Kenya na Rwanda, ambapo Tanzania iliibuka kinara wa ushiriki.
“Katika baadhi ya makongamano, karibu nusu ya wageni walioshiriki walikuwa ni Watanzania, jambo linalothibitisha kasi ya maendeleo ya ushirika nchini na hamasa ya wanachama wetu kushiriki,” amesema Sumbe.
Mwenyekiti huyo alitoa pongezi kwa Serikali kwa uamuzi wake wa kuanzisha Benki ya Ushirika Tanzania, hatua iliyopokewa kwa mikono miwili na wanauushirika nchini. Serikali tayari imechangia zaidi ya shilingi bilioni tano katika kuimarisha benki hiyo, jambo linalowapa matumaini makubwa ya upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wanachama wa ushirika.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa kutambua umuhimu wa ushirika na kuamua kuwekeza kwenye benki ya ushirika. Huu ni ushahidi kuwa Serikali ipo pamoja na wakulima, wajasiriamali na wafanyakazi,” alisema.
Sumbe amesisitiza kuwa ushirika sio chombo cha watu wanyonge kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu, bali ni mfumo madhubuti wa kiuchumi unaotegemea umoja, mshikamano na uwajibikaji. Alitoa wito kwa Watanzania kote nchini kujiunga na vyama vya ushirika ili kufaidika na fursa zinazopatikana kupitia umoja huo.
“Hakuna mafanikio bila mshikamano. Ili uwe na ushirikiano ni lazima kuwe na umoja. Ushirika unajenga misingi hiyo na ndio maana tunasema – jukwaa letu ni chombo cha mabadiliko ya kweli,” amehitimisha.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi