March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPHPA yazindua kifaa cha kisasa kwa ajili ya utambuzi nwa vinasaba vya mimea,wadudu na magonjwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MAMLAKA  ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imezindua rasmi kifaa cha kisasa aina ya MinION, chenye uwezo wa kutambua vinasaba vya mimea, wadudu na magonjwa kwa haraka zaidi .

 Kifaa hicho, chenye uwezo wa  kutoa majibu ndani ya dakika ishirini, kinatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto sugu zinazowakabili wakulima nchini.

Akizungumza kwenye banda la TPHPA katika maonesho ya kilimo ya Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kifaa hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema kuwa ujio wa kifaa hicho ni hatua kubwa katika mapinduzi ya kilimo nchini Tanzania.

 “Kifaa hiki kilibuniwa nchini Uingereza kwa lengo la kutambua virusi vya hatari kama Zika na Ebola. Hata hivyo, baada ya majaribio ya kina, tumejiridhisha kwa asilimia 100 kuwa kina uwezo mkubwa wa kutumika katika sekta ya kilimo kwa ajili ya utambuzi wa wadudu, mimea na magonjwa kwa haraka mno. Tanzania sasa inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutumia teknolojia hii ya hali ya juu kwenye sekta ya kilimo,” ameeleza Prof. Ndunguru.

Prof.Ndunguru amesema kupitia ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), TPHPA imefanikiwa kupata vifaa hivyo 20, ambavyo vitasambazwa katika vituo vya mamlaka hiyo katika kanda zote nchini.

Amesema,vifaa hivyo vitatumika kushirikiana na wataalamu wa kilimo kubaini haraka visababishi vya magonjwa na wadudu hatari, na hivyo kusaidia katika kupambana na milipuko kabla ya kusambaa kwa kiwango kikubwa.

Prof. Ndunguru ameeleza kuwa, kwa kutumia teknolojia hii, Tanzania sasa itakuwa na uwezo wa kuthibitisha ubora wa mazao yake kabla ya kuuza nje ya nchi, hatua itakayoongeza ushindani wa bidhaa za kilimo kwenye masoko ya kimataifa.

Pia kifaa hicho kitasaidia kuzuia uingizwaji wa vyakula kutoka nje ambavyo vinaweza kuwa hatarishi kwa afya ya binadamu na mazingira kwani kifaa hicho kina uwezo wa kubaini viharaishi vilivyopo kwenye chakula.

“Teknolojia hii siyo ya kutumia kwenye kilimo pekee, bali inaweza kusaidia pia kwenye sekta nyingine kama uhifadhi wa mazingira, utafiti wa viumbe vya majini, wanyamapori na hata kwenye afya ya binadamu,” ameongeza Prof. Ndunguru.

“Tunajivunia mafanikio haya ambayo yamewezekana kwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha changamoto za wakulima zinapatiwa ufumbuzi wa kisayansi na wa kudumu.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya ya Mimea kutoka TPHPA, Dkt. Begnius Ngowi, amebainisha kuwa kifaa hicho kwamba kitakuwa msaada mkubwa kwa wakulima waliokuwa wakihangaika kwa muda mrefu na changamoto za magonjwa na wadudu shambani.

Prof.Ndunguru amesema, aaada ya maonesho hayo ya Nanenane, timu ya wataalamu kutoka TPHPA inatarajiwa kuanza zoezi la kuweka kambi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa na wadudu wanaoathiri mazao ya mbogamboga katika eneo hilo maarufu kwa kilimo cha bustani.

 “Kabla ya ujio wa kifaa hiki, ilichukua muda mrefu sana kutoka sampuli kuchukuliwa hadi majibu kutolewa. Hii ilisababisha wakulima kutumia viuatilifu kwa kubahatisha, na mara nyingi hali ilizidi kuwa mbaya. Sasa, kwa kutumia MinION, tunaweza kupata majibu hapohapo shambani ndani ya dakika ishirini na kuamua hatua sahihi za kuchukua,” amesema Dkt. Ngowi.

Akitolea mfano, amesema wakulima wa nyanya wamekuwa wakikabiliwa na mdudu hatari Tuta absoluta maarufu kama Kantangaze, pamoja na wadudu wengine kama whiteflies kwenye matunda na magonjwa ya Batobato na michirizi ya kahawia kwenye mihogo.

Amesema,wadudu hao hufanana kwa macho ya kawaida lakini wana tofauti kubwa za vinasaba zinazohitaji dawa tofauti kwa ajili ya kudhibiti na kwamba kupitia kifaa hicho , itakuwa rahisi kutambua aina husika na kuchukua hatua sahihi.