March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekta ya utalii wa mikutano kupitia Jukwaa la Kitaifa la Wadau yaimarika

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

TANZANIA imechukua hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya utalii wa mikutano, maonesho, makongamano na safari za motisha (MICE), kwa kuandaa Jukwaa la Wadau wa Sekta ya MICE, lililofanyika leo katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha wadau kutoka sekta za utalii, biashara, serikali na taasisi za mafunzo.

Tukio hilo lilifunguliwa rasmi saa 8:30 mchana kwa hotuba kutoka kwa mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, aliyeeleza dhamira ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha sekta ya mikutano barani Afrika. Alisisitiza kuwa utalii wa mikutano ni chanzo muhimu cha mapato ya kigeni, na unatoa fursa kubwa ya kukuza uchumi kupitia wageni wa kimataifa wanaohudhuria matukio makubwa.

Katika jukwaa hilo, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliwasilisha tathmini ya mwenendo wa sekta ya MICE nchini, ikiainisha changamoto zinazokabili ukuaji wa sekta hiyo, pamoja na fursa zinazopatikana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania. Mfano uliotolewa ni ujenzi wa ukumbi mpya wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 5,000 jijini Arusha, hatua inayolenga kuvutia matukio ya kimataifa na kikanda.

Washiriki pia walipata mafunzo maalum kuhusu uzingatiaji wa sheria, taratibu za ununuzi na mikataba, kupitia warsha iliyoendeshwa na taasisi ya UONGOZI Institute, kwa lengo la kuwawezesha waandaaji wa matukio kuelewa mazingira ya kisheria ya kufanya biashara ya mikutano nchini.

Jukwaa hilo pia liliendesha jopo la majadiliano la sera, sheria na kanuni muhimu kwa biashara ya MICE, likiwakutanisha wataalamu kutoka TTB, BASATA, TRA na BRELA. Majadiliano hayo yalilenga kuboresha uratibu baina ya taasisi za serikali, kurahisisha usajili wa biashara na mikataba, na kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji katika sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Mafunzo ya kitaalam kwa waandaaji wa matukio (Event Management Masterclass) yaliyoendeshwa kuanzia Februari hadi Agosti 2025 pia yalitambuliwa, ambapo wahitimu walipewa vyeti vya kutambua uwezo na juhudi zao katika taaluma hiyo. Mafunzo hayo yalitolewa na kampuni ya Popular Links, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta.

Tukio hilo lilihitimishwa kwa Tafrija ya Mchapalo (Networking Cocktail Reception) iliyoanza saa 12:00 jioni, ikiwa ni jukwaa la washiriki kuanzisha ushirikiano wa kibiashara na kushirikiana katika miradi ya baadaye.

Jukwaa hili limeandaliwa na Popular Links kwa kushirikiana na Alliance Française Dar es Salaam na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na limepokelewa kwa pongezi kutoka kwa wadau wengi kama hatua ya kimkakati ya kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya utalii wa mikutano.